Wayemen waandamana jijini Sana'a wakitaka kuondolewa mzingiro
Wananchi wa Yemen jana Jumanne walifanya maandamano nje ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Sana'a, kulaani mzingiro uliowekwa na Saudi Arabia dhidi ya nchi hiyo.
Wakurugenzi na wafanyakazi wa angatua hiyo waliungana na wananchi katika maandamano hayo, yaliyofanyika kwa mnasaba wa kutimia mwaka wa tano tokea uwanja huo wa kimataifa katika mji mkuu Sana'a uwekwe chini ya mzingiro na muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia.
Waandamanaji hao wametoa mwito wa kuondolewa mzingiro huo, ili kuruhusu kuanza tena safari za ndege za abiria, kwa lengo la kuwasafirisha nje ya nchi wagonjwa wanaohitaji huduma maalumu za kiafya.
Takwimu rasmi zinaonesha kuwa, wananchi 95,000 wa Yemen wameaga dunia kutokana na mzingiro huo wa miaka mitano dhidi ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Sana'a.
Februari 2019, dunia iliguswa na kusikitishwa na kisa cha kuaga dunia watoto pacha wa kiume walioungana nchini Yemen, baada ya kushindwa kupelekwa nje ya nchi kutokana na mzingiro wa kila upande wa Saudia na waitifaki wake dhidi ya nchi hiyo maskini.
Mnamo Machi 2015 Saudi Arabia, kwa kushirikiana na Imarati na kwa uungaji mkono wa serikali ya Obama, ilianzisha hujuma ya pande zote dhidi ya watu madhulumu wa Yemen ambao nchi yao ni masikini zaidi katika bara Arabu.
Vita hivyo ambavyo vimeshaua makumi ya maelfu ya watu vinaendelezwa sambamba na muungano huo wa Saudia kutekeleza mzingiro wa nchi kavu, baharini na angani dhidi ya Yemen.