Ansarullah: Marekani inazuia suhulu ya kisiasa katika mgogoro wa Yemen
Msemaji wa Harakati ya Ansarullah ya Yemen amesema Marekani inakwamisha na kuzuia kupatikana suluhisho la kisiasa katika mgogoro unaoikabili nchi hiyo maskini ya Kiarabu inayozongwa na vita na mapigano tokea mwaka 2015.
Muhammad Abdul-Salam amesema hayo katika ujumbe aliotuma jana Jumatano katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter na kuongeza kuwa: Uingiliaji wa Marekani kwa mambo ya ndani ya Yemen kupitia uvamizi wa kijeshi, umepelekea kukanyagwa mamlaka ya kujitawala nchi hiyo.
Abdul-Salam amebainisha kuwa, Marekani ikishirikiana na Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu zimefanya jitihada za kuamilisha harakati na shughuli za makundi ya kigaidi ya al-Qaeda na Daesh (ISIS) nchini Yemen.
Msemaji wa Harakati ya Ansarullah ya Yemen ameongeza kuwa, kiuchumi, wavamizi hao wameliwekea taifa la Yemen mzingiro shadidi ambao umewasababisha matatizo ya kijamii katika hali zote za kimaisha wananchi wa Yemen.
Abdul-Salam ambaye pia ni Mkuu wa Timu ya Mazungumzo ya Yemen ameeleza bayana kuwa, hakuna shaka kuwa nchi inayozuia kupatiwa ufumbuzi wa kisiasa mgogoro wa Yemen ni Marekani.
Msemaji huyo wa Ansarullah hivi karibuni aliyataja madai ya Marekani na waitifaki wake kuhusu kuisaidia kiuchumi Yemen kuwa ni istihzai na masikhara na kueleza kuwa, kama ingeweza Marekani ingewanyima hata hewa wananchi wa nchi hiyo ya Kiarabu.