Ansarullah yazionya US na Saudia zijiandae kupata pigo Yemen
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i74128-ansarullah_yazionya_us_na_saudia_zijiandae_kupata_pigo_yemen
Baada ya Marekani kuondoka kwa madhila na fedheha kubwa nchini Afghanistan licha ya kutumia matrilioni ya dola, Harakati ya Ansarullah ya Yemen imezitaka Marekani na Saudi Arabia ziandae ramani ya njia ya kuondoka Yemen na kuonya kuwa, nchi hiyo ya Kiarabu karibu hivi itageuka na kuwa kaburi la wavamizi.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Aug 31, 2021 13:30 UTC
  • Ansarullah yazionya US na Saudia zijiandae kupata pigo Yemen

Baada ya Marekani kuondoka kwa madhila na fedheha kubwa nchini Afghanistan licha ya kutumia matrilioni ya dola, Harakati ya Ansarullah ya Yemen imezitaka Marekani na Saudi Arabia ziandae ramani ya njia ya kuondoka Yemen na kuonya kuwa, nchi hiyo ya Kiarabu karibu hivi itageuka na kuwa kaburi la wavamizi.

Mohammed Ali al-Houthi, Mwenyekiti wa Kamati Kuu ya Mapinduzi ya Yemen amesema hayo leo Jumanne katika ujumbe aliotuma kwenye mtandao wa Twitter na kuongeza kuwa, Washington, Riyadh na waitifaki wao wanapaswa kuondoka Yemen mara moja ili Wayemen waishi kwa uthabiti pasi na ardhi yao kukaliwa kwa mabavu.

Amesema: Taifa la Yemen halitakubali uvamizi na ukaliaji wa mabavu wa ardhi yake, bila kujali mgogoro na mapigano yanayoshuhudiwa nchini humo yatachukua muda gani. Yemen itageuka na kuwa kaburi kubwa la wavamizi.

Marekani hapo jana ilitangaza kuondoa rasmi askari wake wote nchini Afghanistan baada ya miaka 20 ya kuikalia kwa mabavu nchi hiyo na kusababisha maafa na hasara kubwa. 

Kundi la mwisho la askari wa US likiondoka kwa madhila nchini Afghanistan

Siku chache zilizopita, askari wasiopungua 30 wa muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia waliangamizwa na wengine 60 kujeruhiwa katika shambulio lililofanywa na wapiganaji wa harakati ya Ansarullah dhidi ya kituo kikubwa zaidi cha kijeshi cha muungano huo vamizi kusini mwa Yemen.

Hujuma na mashambulio ya muungano huo vamizi wa kijeshi tokea Machi 2015 yameshaua makumi ya maelfu ya Wayemen, mbali na kuisababishia nchi hiyo masikini ya Kiarabu janga kubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa duniani la maafa ya kibinadamu.