Hamas yapinga masharti ya Marekani kwa shirika la UNRWA
(last modified Fri, 03 Sep 2021 08:04:04 GMT )
Sep 03, 2021 08:04 UTC
  • Hamas yapinga masharti ya Marekani kwa shirika la UNRWA

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas imepinga suala la kuanza tena shughuli za shirika la Umoja wa Mataifa la misaada ya kibinadamu kwa Wapalestina, UNRWA kwa kifupi.

Taarifa iliyotolewa leo Ijumaa na harakati ya Hamas imesema kuwa, makubaliano yaliyotiwa saini baina ya UNRWA na Marekani juu ya kuanza tena himaya ya Washington kwa jumuiya hiyo ya misaada ya kibinadamu kwa Wapalestina yana masharti hatari sana yaliyotolewa na serikali ya Washington.

Hamas imesema kuwa, makubaliano hayo yanakiuka sheria za kimataifa na kanuni za misaada ya kibinadamu na yanaufanya wakala wa Umoja wa Mataifa wa UNRWA kuwa wenzo na fimbo ya kisiasa ya serikali ya Marekani.

Hamas imeitaka UNRWA ijitoe katika makubaliano hayo ambayo imesema yanahatarisha faili la wakimbizi wa Kipalestina.

Mwezi Januari mwaka 2018 serikali ya Marekani ilikata msaada wake wa dola milioni 300 kwa shirika la Umoja wa Mataifa la misaada ya kibinadamu kwa Wapalestina, UNRWA kwa lengo la kuzishinikiza harakati za mapambano ya ukombozi wa Palestina zikubaliane na mpango habithi wa Muamala wa Karne uliobuniwa na serikali ya aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Donald Trump.  

Tags