New York Times: Hizbullah imeishinda na kutoa pigo kwa Marekani
Gazeti la New York Times la Marekani limekiri kuwa harakati ya Hizzbullah ya Lebanon imeibuka na ushindi katika mpambano wake na Marekani.
Makala iliyoandikwa na gazeti hilo la New York Times imesema kuwa, Hizbullah imeipiku na kuishinda Marekani baada ya kuonekana kama muokozi wa taifa nchini Lebanon.
New York Times limeandika kuwa, harakati ya Hizbullah ya Lebanon Alkhamisi iliyopita ilitangaza kuwa, imeingiza nchini humo magaloni milioni moja ya diseli kupitia mpaka wa Syria.
New York Times limendika kuwa, Walebanon wamefurahishwa sana na harakati hiyo ya Hizbullah iliyoikasirisha Marekani kwa upande mmoja, na kukidhi mahitaji muhimu ya nchi hiyo ambayo ilikuwa imedumaa kutokana na uhaba wa mafuta na dizeli kwa upande mwingine.
Makala ya New York Times imesema: Wakati Lebanon ilipokuwa katika msambaratiko mkubwa zaidi wa kiuchumi katika historia ya nchi hiyo, Hizbullah imeweza kujitokeza kama muokozi wa kitaifa na kuweka mguu katika medani ambayo serikali ya Beirut na washirika wake wa Kimagharibi wamefeli na kushindwa.
Vyombo vya habari vya Lebanon, mapema jana vilitangaza kuwa msafara wa kwanza wa mafuta ya Iran uliokuwa na malori 20 ya mafuta umeingia nchini humo.
Msafara huo ulifuatiwa na misafara mingine mitatu yenye malori ya mafuta kutoka Iran.
Jumapili wiki hii, meli kubwa ya mafuta ya Iran ilitia nanga katika bandari ya Baniyas nchini Syria ikiwa imebeba mafuta kwa ajili ya taifa la Lebanon linalosumbuliwa na mzingiro wa kidhalimu wa Marekani, Israel na washirika wao.