Mwito wa kundi la Taliban kwa jamii ya kimataifa
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i74784-mwito_wa_kundi_la_taliban_kwa_jamii_ya_kimataifa
Kundi la Taliban nchini Afghanistan limesema kuwa linataka kuwa na uhusiano mzuri na jamii ya kimataifa. Kundi hilo limesema kuwa, manufaa ya Afghanistan ni manufaa ya jamii ya kimataifa na kusisitiza kwamba, lina hamu ya kuwa na uhusiano mzuri wa kidiplomasia na jamii ya kimataifa.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Sep 18, 2021 03:09 UTC
  • Mwito wa kundi la Taliban kwa jamii ya kimataifa

Kundi la Taliban nchini Afghanistan limesema kuwa linataka kuwa na uhusiano mzuri na jamii ya kimataifa. Kundi hilo limesema kuwa, manufaa ya Afghanistan ni manufaa ya jamii ya kimataifa na kusisitiza kwamba, lina hamu ya kuwa na uhusiano mzuri wa kidiplomasia na jamii ya kimataifa.

Matamshi hayo ya Zabihullah Mujahid, msemaji wa kundi la Taliban kuhusu umuhimu wa kuwepo uhusiano mzuri baina ya kundi hilo na jamii ya kimataifa umetolewa katika hali ambayo Taliban wameingia madarakani kwa mtutu wa bunduki na sasa hivi wanataka kuionesha jamii ya kimataifa kwamba kundi hilo limebadilika na kwamba siasa zake sasa si za kutumia mabavu wala mtutu wa bunduki. Katika kipindi cha siku za hivi karibuni, viongozi wa kundi hilo wamekuwa wakitoa misimamo pamoja na kuandika barua mbalimbali kwa sabaha ya kuomba misaada ya kimatiafa ya kifedha na kiuchumi ya kuwawezesha kuendesha serikali.

Kundi la Taliban limeamua kufuata njia ya kidiplomasia katika upeo wa kimataifa kujaribu kuuthibitishia ulimwengu kuwa Taliban wa hivi sasa sio tena wale Taliban wa miaka 20 iliyopita na sasa hivi wana hamu ya kuachana na vita na umwagaji wa damu. Hata hivyo kinachosubiriwa na duru za kimataifa bali hata ndani ya Afghanistan kwenyewe, ni kuona vitendo vya kundi hilo vinabadilika si maneno tu.

Viongozi waandamizi wa kundi la Taliban

 

Mara baada ya kuiteka Kabul, mji mkuu wa Afghanistan, kundi la Taliban lilitangaza kuwa limekusudia kuunda serikali pana itakayoshirikisha watu wa makundi na matabaka yote ikiwa ni katika juhudi za kuiridhisha jamii ya kimataifa. Lakini si tu halikutekeleza ahadi yake hiyo, bali limeweka pia sheria kali za kukwamisha uhuru wa vyombo vya habari na uhuru wa kisiasa na kiutamaduni katika jamii ya Afghanistan.

Duru za kimataifa zimekuwa zikisema mara kwa mara kwamba vitendo vya kundi la Taliban ndio msingi wa misimamo ya jamii ya kimataifa na kukubalika kwake kisiasa ndani ya Afghanistan. Iwapo litashindwa kufanya hivyo, kundi hilo litawekewa vikwazo ambavyo vitakwamisha utawala wake. 

Asef Ashena, mtaalamu wa masuala ya kisiasa anasema: Katika muongo uliopita, wananchi wa Afghanistan wamepevuka kisiasa, kiuchumi na kiustawi wa kibindamu. Lakini kundi la Taliban halioneshi kuwajali, bali linajali tu aidiolojia zake za utawala ambazo hazina washitiri wengi katika jamii ya Afghanistan na katika upeo wa kimataifa.

Kiujumla ni kwamba kipimo kikuu cha kuweza kukubalika kundi la Taliban ndani ya Afghanistan na pia kieneo na kimtaifa, ni kutambua kwake rasmi mirengo na makundi ya kisiasa, kikaumu na kimadhehebu ya nchi hiyo pamoja na kuheshimu haki za wanawake, uhuru wa vyombo vya habari na harakati za kijamii na za kiraia za wananchi wa Afghanistan.

Hivi sasa kundi la Taliban halioneshi ishara yoyote ya kukubali kugawa madaraka na kushirikisha watu wa kaumu na madhehebu tofauti bali linashikilia baraza lake la mawaziri ambalo haliungwi mkono na kundi lolote la ndani na wala halizivutii kabisa duru za kimataifa. Kila mmoja analiangalia kwa woga baraza hilo na uongozi mpya wa Afghanistan.

Maandamano ya kulalamikia Baraza la Mawaziri la Taliban na kutupwa nje wanawake

 

Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, dunia ya leo iliyopiga hatua za mawasiliano ya Intaneti inatofautiana na dunia ya miaka 20 iliyopita. Hivyo si sahihi kuendesha serikali kwa fikra za miongo miwili iliyopita. Aidiolojia ya kundi la Taliban ni kutoshirikishwa wanawake katika uendeshaji wa nchi. Lakini mwanamke ni kiungo muhimu katika jamii na wana mchango mkubwa katika taasisi kama za elimu na vituo mbalimbali muhimu. Sasa siasa kali zinazotumiwa na Taliban katika kuwabana wanawake kielimu si tu zitapelekea sehemu kubwa ya wananchi wa Afghanistan kukosa elimu lakini pia jamii hiyo itakosa wataalamu katika sekta muhimu ambazo nyingine wanaoziweza ni wanawake, si wanaume.

Narges Itimad, mtaalamu mwingine wa masuala ya kisiasa raia wa Afghanistan anasema: Hakuna mabadiliko yoyote baina ya Taliban wa hivi sasa na wale wa miaka 20 iliyopita. Inavyotakiwa ni kwamba Taliban wavutie kwanza fikra za makundi makubwa ya wananchi wa Afghanistan hata kabla ya kuzivutia duru za kimataifa; na hilo haliwezekani bila ya kuheshimu haki za kiraia za wananchi wa nchi hiyo.

Alaakullihaal, sisitizo la kundi la Taliban la kutaka kuwa na uhusiano mzuri na jamii ya kimataifa ni kitu kinacholeta matumaini mazuri. Kinachopaswa kufanywa sasa na kundi hilo ni kuthibitisha kivitendo nia na hamu yake hiyo.