Ansarullah ya Yemen yaikomboa Ma'rib toka mikononi mwa wavamizi
Harakati ya Ansarullah ya Yemen imefanikiwa kuukomboa mkoa wa kistratajia wa Ma'rib uliokuwa chini ya udhibiti wa muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia.
Vyombo vya habari vya Yemen vimeripoti kuwa, wanamapambano wa Ansarullah wameukomboa mkoa huo wa kistratijia baada ya askari na mamluki wa muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia kusalimu amri, kufuatia mapigano makali baina ya pande mbili.
Habari zaidi zinasema kuwa, kufikia Septemba 23, wapiganaji wa Ansarullah walikuwa wamefanikiwa kukomboa wilaya 10 kati ya 14 za mkoa huo wenye utajiri wa mafuta.
Inaarifiwa kuwa, baada ya harakati ya wananchi ya Ansarullah kudhibiti ngome zote za mkoa wa Ma'rib, imetwaa silaha na zana za kijeshi za muungano vamizi wa Saudia.
Haya yanajiri siku moja baada ya wanajeshi wa muungano vamizi wa Saudia kujisalimisha kwa wanamapambano wa Ansarullah katika wilaya ya Al-Abdiya, kusini mwa mkoa wa Ma'rib.
Mwezi Machi mwaka 2015, Saudi Arabia na waitifaki wake walianzisha mashambulio na uvamizi wa kijeshi dhidi ya Yemen uliosababisha vifo vya makumi ya maelfu ya raia, kuteketeza miundombinu na kuiwekea mzingiro nchi hiyo masikini ya Kiarabu, lakini kutokana na muqawama wa wananchi wa Yemen, hadi sasa wameshindwa kufikia malengo ya uvamizi wao huo.