Saudi Arabia yaweka masharti mapya kwa Waislamu wanaotaka kwenda kufanya Umra
(last modified Mon, 11 Oct 2021 02:30:23 GMT )
Oct 11, 2021 02:30 UTC
  • Saudi Arabia yaweka masharti mapya kwa Waislamu wanaotaka kwenda kufanya Umra

Wizara ya Hija na Waqfu ya Saudi Arabia imetangaza kuwa, itatoa kibali cha kwenda kutekeleza faradhi ya Hija au Umra katika haram mbili tukufu za Makka na Madina kwa wale tu waliopigwa chanjo mbili za kinga ya ugonjwa wa Covid-19 zitakazothibitishwa na nchi hiyo.

Taarifa ya wizara hiyo imeeleza kuwa, uamuzi huo umechukuliwa kulingana na maelekezo ya wizara ya afya ya nchi hiyo kwa madhumuni ya kutekeleza itifaki za kinga za maambukizi ya virusi vya corona ili kulinda afya za Waislamu wanaoelekea nchini humo kwa ajili ya Umra, wanaohudhuria Sala na wanaokwenda kuzuru Masjidul-Haram na Msikiti wa Mtume SAW.

Wizara ya Hija na Waqfu ya Saudi Arabia imeendelea kueleza katika taarifa yake kwamba, ili kuepusha kubatilishiwa kibali cha kuingia nchini humo, wageni wa ardhi tukufu ya wahyi waliopanga kwenda huko kutekeleza Umra au kuzuru maeneo matakatifu lakini wakawa bado hawajapata chanjo kamili ya corona, watatakiwa wawe wameshapata chanjo ya pili masaa 48 kabla, ili kuhakikisha wanapatiwa kibali hicho.

Hija katika mazingira ya maambukizi ya corona

Kwa mujibu wa baadhi ya duru za habari, Saudia itapokea kila siku mahujaji elfu sitini wanaokusudia kutekeleza ibada ya Umra, ikiwa ni takriban mahujaji milioni mbili kwa mwezi.

Ikumbukwe kuwa mnamo mwezi Agosti mwaka huu Saudia ilikataa kupokea Waislamu kutoka nchi 33 duniani wakiwemo Wairani waliokusudia kuzuru haramaini kwa ajili ya kutekeleza ibada ya Umra.

Mwezi Oktoba 2020 serikali ya Riyadh na baada ya kusitisha hija ndogo ya Umra kwa takriban miezi saba kwa sababu ya msambao wa virusi vya corona, ilifungua njia tena ya utekelezaji wa ibada hiyo na kuruhusu kuingia kila siku huko Masjidul Haram mahujaji elfu ishirini, sawa na mahujaji laki sita kwa mwezi.../

Tags