HAMAS yapongeza jitihada za kupokonywa Israel uanachama wa AU
(last modified Mon, 18 Oct 2021 03:53:33 GMT )
Oct 18, 2021 03:53 UTC
  • HAMAS yapongeza jitihada za kupokonywa Israel uanachama wa AU

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) imepongeza na kuunga mkono jitihada zinazoendelea za kuupokonya utawala wa Kizayuni wa Israel kibali cha kuwa mwanachama mtazamaji wa Umoja wa Afrika (AU).

Kiongozi mwandamizi wa HAMAS, Basem Naim alisema jana Jumapili katika taarifa kuwa, harakati hiyo ya muqawama imekaribisha kwa mikono miwili hatua ya Baraza la Utendaji la Umoja wa Afrika ya kuakhirisha mpango wa kuiidhinisha Israel kuwa mwanachama mtazamaji wa AU.

Katika Mkutano wa 39 wa Baraza la Utendaji la Umoja wa Afrika uliofanyika katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa, yalipo makao makuu ya AU, baraza hilo lilitangaza habari ya kuakhirishwa mpango huo hadi Februari mwakani.

Uamuzi wa upande mmoja uliochukuliwa na Mwenyekiti wa Kamisheni ya AU mwezi Julai mwaka huu wa kuupatia utawala wa Kizayuni wa Israel hadhi ya kuwa mwanachama mtazamaji katika taasisi hiyo kuu ya bara la Afrika umelaaniwa ndani na nje ya bara hilo.

Musa Faki Mahamat, Mwenyekiti wa Kamisheni ya AU

HAMAS imesema uamuzi huo wa AU si tu utaupa uhalali utawala ghasibu wa Israel wa kuendelea kupora ardhi zaidi za Wapalestina, lakini pia utaushajiisha na kuupa nguvu utawala huo haramu ya kuendelea na njama yake ya kutaka kufuta haki za Wapalestina.

Harakati hiyo ya mapambano ya Kiislamu ya Palestina inasisitiza kuwa, kuuidhinisha utawala pandikizi wa Israel kuwa mwanachama mtazamaji wa taasisi hiyo kubwa zaidi ya kibara ni sawa na kuubariki utawala huo uendeleze jinai zake dhidi ya wananchi wa Palestina.

 

Tags