Israel yaingiwa na kiwewe cha kulipiziwa kisasi na muqawama wa Palestina
Jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel limefunga kambi na njia za kuelekea maeneo ya karibu na Ukanda wa Ghaza huko Palestina kwa kuhofia ulipizaji kisasi wa muqawama wa Palestina kutokana na jinai za kila siku za Wazayuni.
Hayo yameripotiwa na shirika la habari la IRNA ambalo limemnukuu Avichay Adraee, msemaji wa jeshi la utawala wa Kizayuni akisema kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba, jeshi la Israel limelazimika kufunga njia za maeneo ya karibu na Ukanda wa Ghaza pamoja na kambi zake za kijeshi kwa kutegemea taarifa maalumu ilizo nazo. Pamoja na hayo lakini amesema, hadi hivi sasa hakujatolewa amri yoyote ndani ya utawala wa Kizayuni kuhusu vitongoji vilivyoko karibu na Ukanda wa Ghaza.
Tovuti ya Kizayuni ya "Walla" nayo imemnukuu afisa mmoja wa ngazi za juu wa jeshi la Israel akisema kuwa, tathmini zinaonesha kwamba, hatua hizo za kiusalama kwenye mpaka wa Ghaza zimechukuliwa kabla ya kutangazwa bajeti kuu ya utawala wa Kizayuni.
Nago gazeti la Kizayuni la Haaretz limenukuu duru moja ya Ukanda wa Ghaza ikisema kuwa, jeshi la Israel limeamua kuchukua hatua hizo za kiusalama kutokana na wahka na hofu yake kubwa kuhusu makombora ya kusambaratisha vifaru pamoja na wapiga shabaha stadi wa muqawama wa Palestina na hatari za kiusalama katika maeneo ya karibu na Ukanda wa Ghaza.
Hatua hizo za utawala wa Kizayuni zimechukuliwa baada ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS kusema kuwa, jinai za utawala wa Kizayuni hazitoachwa zipite vivi hivi, na iwapo Israel itaendelea kuzuia misaada kuingia Ukanda wa Ghaza, basi ijiandae na vipigo vingine kutoka kwa muqawama wa Palesitna.