Bahrain yakataa kumuachia huru mtoto wa miezi 17
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i7738-bahrain_yakataa_kumuachia_huru_mtoto_wa_miezi_17
Serikali ya Bahrain imekataa ombi la mfungwa wa kisiasa Zainab al-Khawaja, kumuachia huru mwanawe wa miezi 17, kwa kuwa hali yake imedhoofu na hawezi tena kumshughulikia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 24, 2016 11:51 UTC
  • Bahrain yakataa kumuachia huru mtoto wa miezi 17

Serikali ya Bahrain imekataa ombi la mfungwa wa kisiasa Zainab al-Khawaja, kumuachia huru mwanawe wa miezi 17, kwa kuwa hali yake imedhoofu na hawezi tena kumshughulikia.

Kituo cha Kutetea Haki za Binadamu cha Ghuba ya Uajemi PGCHR kimesema vyombo vya dola nchini Bahrain vimekataa kumruhusu mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 31 kumkabidhi mwanawe kwa babake huku maafisa wa gereza wakisisitiza kuwa 'jambo hilo haliruhusiwi'. Habari zaidi zinasema kuwa, maafisa wa gereza anakozuiliwa mfungwa huyo wa kisiasa wamemnyima idhini Khadija al-Mousawi, bibi wa mtoto kumuona mjukuu wake huyu. Bibi huyo amekiambia kituo hicho cha kutetea haki za binadamu kuwa: "Inaelekea kuwa sio tu binti yangu Zainab amefungwa jela, bali pia mjukuu wangu Abdulhadi."

Khawaja anatumikia kifungo cha miaka mitatu na nusu jela, baada ya kupatikana na hatia ya kuchana picha ya Hamad bin Isa Al Khalifa, Mfalme wa utawala wa Aal-Khalifa. Mwanamke huyo ni binti ya Abdulhadi al-Khawaja, mwanaharakati mashuhuri wa Bahrain ambaye kwa sasa anatumikia kifungo cha maisha jela, baada ya kupatikana na hatia ya eti kujaribu kuipindua serikali ya Manama. Chama kikuu cha upinzani nchini humo cha al-Wefaq karibuni hivi kilitoa ripoti iliyosema kuwa, vyombo vya usalama vya Bahrain vimekamata watu 1,765 wakiwemo watoto wadogo 120 tokea mwaka jana 2015 hadi sasa, kwa lengo la kukandamiza maandamano ya amani ya wananchi wanaopinga dhulma za utawala wa Manama.