Palestina, kipaumbele muhimu zaidi cha Ulimwengu wa Kiislamu
Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge) amesema kuwa kadhia ya Palestina ndio kipaumbele kikubwa zaidi cha Ulimwengu wa Kiislamu na kwamba kambi ya muqawama na mapambano ndiyo sababu ya kudhalilishwa na kuchukiwa Wazayuni.
Muhammad Qalibaf aliyasema hayo katika Mkutano wa 16 wa Jumuiya ya Mabunge ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) unaofanyika nchini Uturuki ambao umejikita zaidi katika suala la Afghanistan. Amesema, katika miongo ya karibuni nchi za Waislamu zilianzisha harakati mpya za ustawi katika nyanja mbalimbali za kiutamaduni, kijamii na kisiasa na kuongeza kuwa, mabadiliko hayo ya taratibu yatazaa matunda ya mustakbali mwema kwa Ulimwengu wa Kiislamu pale mataifa yote ya Waislamu yatakaposhirikiana na kushikamana kwa kutumia maadili ya Kiislamu kwa ajili ya kutatua matatizo ya Umma wa Kiislamu. Amesisitiza kuwa, kudumishwa njia hiyo kutapelekea kuangamizwa utawala wa Kizayuni wa Israel.
Akibainisha kwamba, kadhia ya Palestina ndiyo kipaumbele cha kwanza cha Ulimwengu wa Kiislamu, Muhammad Qalibaf amesema: "Imepita zaidi ya miongo saba sasa ambapo dunia inatazama kwa macho tu siasa na ukatili wa utawala wa Kizayuni wa Israel unaokiuka misingi ya awali kabisa ya haki za binadamu na utu wa Wapalestina."
Amehoji kwamba, je, nchi za Kiislamu zimechukua hatua gani ya maana katika uwanja huu? Hili ni swali linalopaswa kujibiwa katika hali ya hivi sasa ya wananchi wa Palestina na kuendelea dhulma na uvamizi Israel dhidi ya taifa hilo.
Kuwaunga mkono wananchi wa Palestina kuna mambo mawili muhimu; la kwanza ni kuunga mkono muqawama na mapambano dhidi ya wavamizi ili kukomesha dhulma ya kihistoria inayofanyika huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Suala la pili ni ulazima wa kuwepo mshikamano wa kweli baina ya nchi za Kiislamu ili kutatua matatizo ya Ulimwengu wa Kiislamu. Akisisitiza nukta hiyo, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa umoja, mshikamano na kushirikiana baina ya Waislamu ni maudhui ya kistratijia ya Umma wa Kiiislamu na kuongeza kuwa, suala hilo muhimu linapaswa kupewa mazingatio maalumu na Jumuiya ya Mabunge ya Nchi za Kiislamu.
Matukio ya Palestina yanaonesha kuwa, ukimya na kutochukua hatua haviwezi kutokomeza dhulma inayofanywa dhidi taifa lolote lile; kwani chini ya kimya hicho, kila kitu cha taifa la Palestina, ikiwemo ardhi yake, heshima yake na utambulisho wake, vimetwaliwa na wavamizi. Katika uvamizi huo wa wazi, utawala ghasibu wa Israel umekiuka misingi ya sheria za Umoja wa Mataifa na kuwalazimisha Wapalestina zaidi ya milioni 5 kuwa wakimbizi. Tangu ulipoasisiwa kwa njia haramu mwaka 1948, utawala huo dhalimu umekuwa ukifuatilia malengo mawili:
Lengo la kwanza ni kupata uhalali huku ukiwa utawala vamizi, jambo ambalo halijafanikiwa; kwa sababu muqawama na mapambano ya Palestina yanaendelea kutoa changamoto kubwa ya kupinga uhalali wa utawala ghasibu wa Israel.
Sheikh Maher Hammoud, Rais wa Jumuiya ya Kimataifa ya Maulamaa wa Muqawama huko Lebanon anasisitiza kuwa, Quds na Palestina ni suala la kwanza na kuu la Ulimwengu wa Kiislamu na kuongeza kuwa: Ushindi wa Hizbullah mwaka 2006 na mafanikio ya wanamapambano wa Gaza mwaka 2009, 2012 na 2014 vilipelekea kufeli na kushindwa njama ya Marekani na Israel ya kubadilisha mipaka ya kijiografia ya nchi za Kiislamu.
Lengo la pili la Israeli ni kutaka kuidhibiti Baitul Muqaddas ambayo ni kibla cha kwanza cha Waislamu na kuharibu utambulisho wa kihistoria wa taifa la Palestina. Katika mwendelezo wa mchakato huo, Marekani na utawala wa Kizayuni wanataka kadhia ya Palestina isahaulike milele kupitia njama ya kuanzisha uhusiano kati ya utawala huo dhalimu na tawala za Kiarabu.
Hapana shaka kwamba, haki ya kurejea Wapalestina katika ardhi na nchi yao, haki ya kujitawala na haki ya kuanzisha dola huru la Palestina yote ni masuala muhimu yanayohusu haki za watu wa Palestina ndani ya fremu ya sheria za kimataifa.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaamini kwamba, amani ya kiadilifu na shirikishi haiwezi kupatikana duniani isipokuwa kwa njia ya kukomesha dhulma na mabavu, kuheshimu haki za mataifa yote, maadili ya kidini na kitamaduni na kufuata kanuni ya kujitawala kwa mataifa mbalimbali.