Hamas yamshukuru mcheza tenisi Mkuwaiti aliyekataa kucheza na Mzayuni
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) imempongeza mcheza tenisi wa Kuwait aliyekataa kucheza na mwakilishi wa utawala wa Kizayuni wa Israel.
Tarehe 21 Januari mcheza tenisi kijana wa Kuwait, Mohammad Al-Awadi alikataa kucheza dhidi ya mwakilishi wa utawala wa Kizayuni wa Israel baada ya kushinda mechi ya nusu fainali ya Mashindano ya Tenisi ya Dunia chini ya umri wa 14 akitangaza uungaji mkono wake kwa watu wa Palestina. Hatua hiyo imepongezwa sana kwenye mitandao ya kijamii ya Kiarabu na vyombo vya habari.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Fars, msemaji wa harakati ya Hamas, Hazem Qasim, amepongeza hatua ya Mohammad Al-Awadi na kusema: "Hatua ya kijana huyu wa Kuwait imetokana na dhamiri ya Umma wa Kiislamu na inaoana na misingi ya heshima na izza."
Msemaji wa Hamas amesisitiza kuwa, kitendo cha mcheza tenisi wa Kuwait kimepelekea kushindwa ndoto za kutaka kutokomeza malengo matukufu ya Palestina katika nyoyo za watu wa Kuwait.
Awali Dawood Shahab mmoja wa viongozi wa harakati ya Jihad Islami ya Palestina, alisema kuwa: "Kwa kujiondoa kwenye mchezo dhidi ya mpinzani Mzayuni, Mohammad Al-Awadi ameandika jina lake katika historia na atatambuliwa kwa vyeo vya heshima na izza dhidi ya sera za kutaka kufanya mapatano na adui Mzayuni."