Vipengee vya kimkakati katika matamshi ya Sayyid Hassan Nasrullah
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i80156-vipengee_vya_kimkakati_katika_matamshi_ya_sayyid_hassan_nasrullah
Mahojiano maalumu ya televisheni ya Al-Alam na Katibu Mkuu wa harakati ya Hizbullah ya Lebanon Sayyid Hassan Nasrallah, Jumanne jioni, kuhusu hali ya ndani ya Lebanon na matukio ya kikanda na kimataifa, yamepewa mazingatio katika vyombo vya habari vya kimataifa kutokana na vipengee vya masuala ya kistratijia yaliyojadiliwa katika mahojiano hayo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 09, 2022 07:09 UTC
  • Sayyid Hassan Nasrullah
    Sayyid Hassan Nasrullah

Mahojiano maalumu ya televisheni ya Al-Alam na Katibu Mkuu wa harakati ya Hizbullah ya Lebanon Sayyid Hassan Nasrallah, Jumanne jioni, kuhusu hali ya ndani ya Lebanon na matukio ya kikanda na kimataifa, yamepewa mazingatio katika vyombo vya habari vya kimataifa kutokana na vipengee vya masuala ya kistratijia yaliyojadiliwa katika mahojiano hayo.

Matamshi ya Katibu Mkuu wa Hizbullah kwa mara nyingine tena yamefichua baadhi ya mambo na njama zinazofanyika nyuma ya pazia; suala ambalo lina umuhimu si kwa viongozi wa nchi, wanasiasa, wanaharakati na wadau wa vyombo vya habari pekee, bali hata kwa fikra za waliowengi ndani na nje ya Lebanon. Matamshi hayo yamebatilisha vitisho vya hivi karibuni vya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Lebanon na kambi ya mapambano kwa ujumla. 

Katika mahojiano hayo Sayyid Nasrullah alihoji kwamba, je, Israel inajua idadi kamili ya makombora ya Hizbullah na maeneo yaliko? na kusema: "Huko nyuma Hizbullah haikunyamazia kimya mashambulizi ya Israel kwenye maeneo yasiyo na raia nchini Lebanon, sasa itakuwa vipi iwapo utawala huo wa Kizayuni utalenga ngome halisi za Hizbullah?! Hizbullah haitaki kuingia vitani lakini haiogopi vita." 

Wapiganaji wa Hizbullah

Jambo jingine lililowekwa wazi kwa mara ya kwanza na Katibu Mkuu wa Hizbullah ni kuhusu uwezo wa ulinzi wa anga wa harakati hiyo. Sayyid Nasrullah amesema: Awali Hizbullah ilikuwa imetangaza kuwa, itatungua ndege zisizo na rubani za Israel na jambo muhimu ni kwamba tishio la ndege hizo kwa Lebanon sasa limeondoka. Kwa msingi huo Muqawama na Hizbullah imeanza kutumia silaha ya ulinzi wa anga. Tangu tulipoanza kutumia silaha za aina hiyo harakati za ndege zisizo na rubani za utawala wa Kizayuni katika anga ya Lebanon zimepungua kwa kiasi kikubwa sana. Ubora na kiwango cha nguvu za kijeshi za Hizbullah na uwezo wake ambao hauna kifani katika historia ya Lebanon bali hata katika historia ya harakati za mapambano dhidi ya adui vimeipa harakati hii nguvu na uwezo wa kutoshindwa katika vita vyovyote."

Katibu Mkuu wa Hizbullah ametilia mkazo utambulisho wa Kilebanon wa harakati hiyo kwa ajili ya kutimiza matakwa ya wananchi na kutatua matatizo yao na kusema: "Hizbullah, kuanzia makamanda wake hadi wapiganaji na familia zao ni Walebanon na ni sehemu ya historia na muundo wa jamii wa nchi hii. Maamuzi ya Hizbullah pia ni ya Kilebanoni na yanachukuliwa kwa mujibu wa maslahi ya watu wa Lebanon, lakini wakati huo huo ni muitifaki wa Iran."

Katika sehemu nyingine, Sayyid Hassan Nasrullah amefichua harakati zinazofanyika ndani ya ubalozi wa Marekani mjini Beirut na njama za baadhi ya wanasiasa wa Lebanon kwa maagizo na amri za ubalozi huo na kusema: Wale wanaofanya njama kutokana na maagizo ya ubalozi wa Marekani mjini Beirut hebu watueleze tangu mwaka 2015 wamefanya nini kwa nchi hii zaidi ya mapigano na kuiweka nchi kwenye ncha ya kutumbukia kwenye vita vya ndani? Watu hawa hawana sera na mipango ya kuiokoa Lebanon isipokuwa kuhujumu Hizbullah na Iran." Sayyid Nasrullah amesema ubalozi wa Marekani unaingilia masuala ya uchaguzi wa Lebanon.

Sayyid Hassan Nasrullah

Ingawa kwa sasa Marekani haiikalii kwa mavu ardhi ya Lebanon lakini inaingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo na ina ushawishi wa kisiasa, kifedha na kijeshi katika nchi hiyo. Mfumo wa benki wa Lebanon ni tegemezi kwa maamuzi ya Wizara ya Fedha ya Marekani. Katibu Mkuu wa Hizbullah amesema: "Jengo la ubalozi wa Marekani mjini Beirut linatumiwa na shirika la ujasusi la nchi hiyo CIA kama kituo cha ujasusi cha baadhi ya nchi za Mashariki ya Kati na unatumiwa kusajili majasusi kwa maslahi ya utawala wa Kizayuni wa Israel. Wamarekani wamefanya jitihada za kuzungumza na Hizbullah lakini sisi hatukubali kuzungumza na adui."

Sehemu nyingine ya mahojiano ya Sayyid Hassan Nasrullah na televisheni ya al Alam inahusiana na kadhia ya kuchora na kuainisha mipaka ya majini ya Lebanon na utawala haramu wa Israel kwa upatanishi wa Marekani na Umoja wa Mataifa. Amesema: "Hizbullah haiingilii suala la kuainisha mipaka na jambo hilo linaihusu serikali ya Lebanon. Hata hivyo Hizbullah inatoa sharti moja kuu nalo ni kwamba suala hilo lisitumiwe kama chombo cha kuanzisha uhusiano na ushirikiano na adui Mzayuni."

Katibu Mkuu wa Hizbullah pia ameashiria sherehe zinazoendelea hapa nchini za ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na kusema: Siku ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran ni miongoni mwa siku adhimu za Mwenyezi Mungu. Iran ni mfano wa kuigwa wa nchi inayojitawala na yenye uhuru kamili ambako wananchi wanawachagua wawakilishi wao; wakati nchi nyingi za Magharibi mwa Asia zinazodai kuwa huru na kujitawala ni tegemezi kwa balozi za nchi ajnabi."

Sayyid Nasrullah amekariri kuwa vita vyovyote dhidi ya Iran vitasababisha mlipuko mkubwa katika eneo la Magharibi mwa Asia na kwamba kipaumbele cha Marekani kwa sasa si vita na Iran bali ni makabiliano na Russia na China. Amesema Iran imeazimia ipasavyo kujibu tishio lolote na haifanyi mzaha na yeyote.

Kwa utaratibu huo, matamshi ya Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon kwa mara nyingine tena yamepewa mazingatio na vyombo vya habari na maoni ya umma kwa sababu yalikuwa na nukta muhimu za kimkakati na kistratijia zinazobainisha mabadiliko ya kimsingi katika mlingano wa nguvu kwenye eneo la Asia Magharibi.