HRW: Kila saa moja Myemen mmoja anauawa au anajeruhiwa
(last modified Sat, 12 Feb 2022 06:51:46 GMT )
Feb 12, 2022 06:51 UTC
  • HRW: Kila saa moja Myemen mmoja anauawa au anajeruhiwa

Shirika la kimataifa la haki za binadamu la Human Rights Watch limetoa ripoti mpya na kusema kuwa, katika mwezi ulioisha wa Januari, kwa kila saa moja kwa uchache Myemen mmoja alikuwa anauawa au anajeruhiwa. Hao ni raia wa kawaida wa Yemen ambao hawahusiki kivyovyote na masuala ya kijeshi.

Leo Jumamosi, shirika la habari la Anadolu limenukuu ripoti ya Human Rights Watch ikisema kuwa, mwezi ulioisha wa Januari, ndio uliokuwa mwezi wa umwagaji mkubwa zaidi wa damu za raia wa Yemen tangu wavamizi walipoivamia nchi hiyo ya Kiarabu miaka saba iliyopita.

Ripoti ya shirika hilo la kimataifa la haki za binadamu imesema kuwa, kuanzia tarehe 6 Januari hadi tarehe pili mwezi huu wa Februari 2022, zaidi ya watu wazima 200 raia wa Yemen na watoto 15 wameuawa na zaidi ya watu wazima 354 wa Yemen na watoto wadogo 30 wamejeruhiwa katika mashambulizi ya wavamizi wanaoongozwa na Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati).

Wahanga wakuu wa jinai za wavamizi wa Yemen wanaoongozwa na Saudia na Imarati ni wananchi wa kawaida

 

Kwa upande wake, Shirika la Haki za Binadamu la Kuokoa Watoto limesema, idadi ya Wayemen waliouawa mwezi ulioisha wa Januari ni mara tatu zaidi ya wastani wa kila mwezi wa mauaji waliyokuwa wanafanyiwa raia huo mwaka jana 2021.

Mkurugenzi wa Shirika la Kuokoa Watoto wa Yemen amesema, wakati wa kuendelea kukaa kimya umeisha. Haiwezekani kuendelea kuangalia kwa macho tu jinsi watoto wadogo wanavyouawa na kujeruhiwa katika mashambulizi huko Yemen.

Katika kipindi cha hivi karibuni, wavamizi wa Yemen wakiongozwa na Saudia na Imarati wameshadidisha sana mashambulizi yao kwenye maeneo ya raia nchini humo.

Tags