Magaidi wanne wakufurishaji watiwa nguvuni mkoani al Anbar, Iraq
Vikosi vya usalama vya Iraq vimewatia nguvuni magaidi wanne wakufurishaji wa genge la Daesh (ISIS) katika operesheni waliyofanya katika mkoa wa al Anbar wa magharibi mwa nchi hiyo.
Jeshi la Iraq linaendelea na operesheni mbalimbali dhidi ya magaidi wa kundi la Daesh katika maeneo tofauti ya nchi hiyo huku jeshi hilo likianzisha awamu mpya ya operesheni za kijeshi za kuangamiza mabaki ya magaidi hao wakufurishaji.
Jeshi la Iraq hivi sasa linaendesha operesheni kubwa katika mkoa wa al Anbar magharibi mwa nchi hiyo kwa lengo la kuwasaka na kuwatia mbaroni mabaki ya magaidi wakufurishaji wa Daesh mkoani huo.
Hii ni katika hali ambayo vyombo vya habari vya Iraq awali viliripoti kuwa, vikosi vya usalama vya nchi hiyo vimefanikiwa kuwagundua na kuwatia nguvuni mamluki sita wa Daesh katika mikoa mitatu ya Nainawa, Baghdad na al Anbar.

Mwaka 2017 baada ya kuendesha mapambano kwa miaka mitatu; Iraq hatimaye ilitangaza ushindi dhidi ya genge la kigaidi na ukufurishaji la Daesh hata hivyo mamluki na masalia ya magaidi wa genge hilo bado wapo katika baadhi ya maeneo ya mikoa ya Diyala, Kirkuk, Nainawa, al Anbar na Baghdad.
Jeshi la Iraq na kikosi cha kujitolea cha wananchi wa Iraq maarufu kwa jina la al Hashdu Shaabi wanaendelea kuwasaka, kuwafurusha na kuwaangamiza magaidi hao wa Daesh huko Iraq ili kuzuia kuibuka tena genge hilo la kigaidi na ukufurishaji lililoundwa na kupewa mafunzo na madola ya kibeberu hasa Marekani.