Maandamano makubwa ya kupinga Israel nchini Uturuki
Ni jambo lisilo na shaka kwamba, nukta dhaifu zaidi kwa kila mwanasiasa ni kulazimika kumueleza adui yake mambo yake ya siri na kumfanya adui huyo aelewe nini hasa kinachotakiwa na mwanasiasa huyo.
Katika hali ambayo, Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki alikuwa akijaribu kuwaonesha watu kwamba ameifanya nchi yake kuwa dola kubwa la kiuchumi, kisiasa na kijeshi katika eneo la Asia Magharibi kiasi kwamba madola makubwa duniani yanalazimika kuomba idhini kwanza kwa Uturuki kabla ya kuweka mikataba yoyote na nchi za ukanda huu, hivi sasa na bila ya kutarajia, mwanasisa huyo amekumbwa na matatizo mengi ya ndani ya nchi na kufelisha madai yake yote ya miaka iliyopita. Hivi sasa anarudi nyuma hatua kwa hatua katika kaulimbiu zake za huko nyuma.
Kuzidi Erdogan kulegeza kamba katika misimamo yake ya huko nyuma, kumeshuhudiwa wazi katika safari za maafisa na viongozi mbalimbali wa Uturuki katika nchi kama za Marekani na Uturuki na mwenyewe Erdogan kuomba fursa ya kuzitembelea Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu na nchi nyingine ambazo huko nyuma zilikuwa ni maadui wa Uturuki ambazo zilimtambua Erdogan na serikali yake kuwa kiranja wa kuongoza mapinduzi dhidi ya tawala za nchi hizo. Si hayo tu, lakini Erdogan amekwenda kwenye hatua mbaya ya kumwalika rasmi rais wa utawala wa Kizayuni kuitembelea Uturuki ambaye naye ameitikia kivitendo mwaliko huo wa Erdogan.
Isaac Herzog, rais wa utawala wa Kizayuni wa Israel alifanya ziara rasmi nchini Uturuki siku ya Jumatano, akapokewa na Rais Recep Tayyip Erdogan ambaye aliitaja ziara hiyo ya siku mbili ya rais wa utawala wa Kizayuni huko Uturuki kuwa ya kihistoria.
Kuporomoka thamani ya sarafu ya taifa ya Uturuki na kupungua nafasi za ajira sambamba na kuongezeka idadi ya watu wasio na kazi na mfumko wa bei za bidhaa nchini Uturuki, mambo hayo yamesababisha matatizo ya kimaisha kwa wananchi wa Uturuki kiasi kwamba wanashindwa hata kushibisha matumbo yao.
Ni vyema kusema hapa kwamba, Rais Recep Tayyip Erdogan ni kati ya wanasiasa wachache wa Uturuki ambaye amekaa muda mrefu madarakani na kuvunja rekodi katika jambo hilo. Hii ni kusema kuwa, kwa kipindi cha miongo miwili mfululizo, Erdogan amekuwa akishikilia uongozi wa nchi hiyo ya Waislamu yaani tangu tarehe 14 Machi 2003 hadi hivi sasa.
Katika muda wote huu wa miongo miwili mwanasiasa huyo wa Uturuki amekuwa akijigamba kuwa ni kiranja wa kuliunga mkono na kulihami taifa la Palestina. Mwaka 2009 wakati akiwa Waziri Mkuu wa Uturuki, Erdogan alionesha msimamo mkali sana dhidi ya Israel wakati wa mkutano wa Baraza la Kimataifa la Uchumi mjini Davos, Uswisi. Alimshambulia wazi wazi kwa maneno rais wa wakati huo wa utawala wa Kizayuni kutokana na jinai za kijeshi za Israel katika Ukanda wa Ghaza na hapo hapo alimwambia mwendeshaji wa mkutano huo kwamba: Mimi siwezi kuendelea kuwepo kwenye mkutano huu.
Mivutano baina ya Uturuki ya Erdogan na utawala wa Kizayuni iliendelea kiasi kwamba, wanajeshi wa Israel waliizamisha meli ya Uturuki iliyokuwa inawapelekea misaada ya kibinadamu wananchi wa Ghaza huko Palestina mwaka huo huo wa 2009. Hata hivyo kuanzia mwaka 2018, uhusiano wa Uturuki na utawala wa Kizayuni ulianza kuwa mzuri na viongozi wa pande mbili walianza kutembeleana na kuporomosha madai yote ya Erdogan na serikali yake ya kulionea huruma na kulitetea taifa linalodhulumiwa la Palestina.
Amma tukija katika suala la ziara ya siku mbili za Jumatano na Alkhamisi ya rais wa utawala wa Kizayuni wa Israel huko Uturuki ni kwamba, ziara hiyo si tu haikumpunguzia Erdogan matatizo yanayomkabili, bali imeyaongeza. Kwa mfano, Temel Karamollaoğlu, Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi cha Kiislamu cha Saadet cha Uturuki, alitoa mwito kwa wananchi Waislamu wa nchi hiyo kujitokeza kwa wingi kulaani ziara ya rais wa utawala wa Kizayuni nchini mwao. Kaulimbiu ya maandamano hayo ilikuwa ni: "Madhalimu wanafanya nini nchini Uturuki?" Maandamano hayo yalifanyika katika miji mbalimbali ya Uturuki kulaani ziara ya rais wa Israel nchini humo.
Nukta ya kutiliwa maanani hapa ni kwamba, tangu mwaka 2008 yaani katika kipindi cha zaidi ya miaka 15 iliyopita, hii ni mara ya kwanza kwa Mzayuni anayedaiwa ni rais wa Israel, kuitembelea Uturuki. Ukweli ni kuwa wananchi wa Uturuki wameonesha wamekubaliana na ziara ya Erdogan katika nchi za Kiarabu, lakini kamwe hawako tayari kuona nchi yao ina uhusiano na utawala wa kibaguzi, pandikizi na dhalimu wa Israel.