Kukosoa Iran ukiukaji wa haki za binadamu nchini Saudi Arabia
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, unyongaji kiholela na vitendo vya ukandamizaji vinavyofanywa na utawala wa Aal Saud siyo njia ya utatuzi wa migogoro ya kujitengezea na kwamba, utawala huo hauwezi kutumia mambo mbalimbali kwa ajili ya kufunika mparaganyiko, matatizo ya kisiasa, kimahakama na ukandamizaji dhidi ya raia.
Saeed Khatizadeh, msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran alisema hayo Jumapili ya juzi katika radiamali yake kwa kunyongwa makumi ya raia nchini Saudi Arabia na kueleza bayana kwamba, hatua hiyo isiyo ya kibinadamu inakinzana wazi na misingi pamoja na vigezo vya awali vya haki za binadamu. Aidha Khatibzadeh amesema kuwa, vitendo hivyo ni kinyume kabisa na vigezo vya kisheria na kimahakama vinavyotambuliwa.
Jumamosi ya majuzi utawala wa Aal-Saud nchini Saudi Arabia katika kipindi cha saa 24 ulietekeleza hukumu ya kifo kwa kuwanyonga wafungwa 81 waliokuwa wanahusishwa na madai ya ugaidi. Shirika rasmi la habari la serikali ya Riyadh lilitangaza hayo na kueleza kuwa, miongoni mwa wafungwa walionyongwa wapo raia saba wa Yemen na mmoja wa Syria. Kwa mujibu wa shirika hilo, wafungwa hao wanadaiwa kufanya jinai mbalimbali, kama vile mauaji na kuwa wanachama wa makundi fulani ya kigaidi. Kunyongwa watu 81 ndani ya muda wa saa 24 kumepiku idadi ya watu wote walionyongwa na watawala wa Aal-Saud ndani ya mwaka mzima wa 2021 nchini Saudia.
Kimsingi Sauudi Arabia ina faili jeusi katika suala zima la haki za binadamu na katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni nchini humo kumeripotiwa matukio mbalimbali ya kunyonga raia, kuwatesa, kamatakamata ya kiholela, kushikiliwa wanaharakati wa masuala ya kisiasa na haki za binadamu bila sababu ya maana sambamba na ukandamizaji dhidi ya raia wasio na hatia yoyote ghairi ya kukosoa tu utawala huo.

Mfano wa wazi wa vitendo vya ukandamizaji vya utawala wa kifamilia wa Aal Saud ni hatua yake ya mwaka 2019 ambapo iliwanyonga wafungwa 37 wakiwemo vijana wadogo sita, ambao walitiwa mbaroni katika maandamano ya amani ya mwaka 2011. Oktoba 12 mwaka 2019, Hussein bin Abdul-Aziz Aal Ribh mfungwa wa Kishia mkazi wa Qatif aliaga dunia gerezani baada ya kuteswa vibaya na askari magereza.
Baada ya Muhammad bin Salman kuteuliwa mwaka 2017 kuwa mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudia, utawala huo umefanya hima ya kuonyesha taswira chanya ya bin Salman kwa walimwengu na kumtambulisha kama mtu aliyefungua ukurasa mpya katika historia ya kisiasa ya Saudia ambaye anafuatilia suala la kuleta mageuzi ya kijamii na haki za binadanmu nchini humo.
Hata hivyo Muhammad bin Salman, mrithi kijana wa kiti cha ufalme wa Saudia, ameonyesha utambulisho wake halisi na kupitia hatua alizochuku na amethibitisha kwamba, badala ya kuwa malengo yake ni kuleta mageuzi ya kweli, amekusudia kuwafuta na kuwatokomeza wapinzani na hata mahasimu wake kupitia mageuzi ya kidhahiri sambamba na madai ya kupambana na ufisadi. Ni kwa muktadha huo ndio maana ameshadidisha mbinyo na ukandamizaji ndani ya Saudi hususan dhidi ya wanaharati wa Kishia.
Sarah Leah Whitson, Mkuu wa Shirika la Msamaha Duniani la Amnesty International Kanda ya Mashariki ya Kati anasema: Kunyongwa kwa umati ambako hakujawahi kutokea na vilevile uendeshaji wa kesi bandia nchini Saudia ni mambo ambayo yameweka wazi madai ya uongo ya Muhammad bin Salman, mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudia kuhusiana na kuiletea mageuzi nchi hiyo.
Ukandamizaji dhidi ya wanaharakati wa masuala ya kisiasa, kiraia na wapinzani wa serikali ya Riyadh haujakomea tu ndani ya nchi hiyo bali umevuka mipaka na kuwasakama wapinzani wa Aal Saud walioko nje ya nchi hiyo. Mfano wa wazi wa hilo, ni mauaji dhidi ya Jamal Khashoggi, mwanahabari na mkosoaji wa Saudia ambaye aliuawa kinyama ndani ya ubalozi mdogo wa Saudi mjini Istanbul Uturuki.
Saudia inaendelea kutoa kiholela na bure bilashi hukumu za kunyongwa wanaharakati wa masuala ya kijamii na wakosoaji wa utawala huo katika hali ambayo, jamii ya kimataifa na madola ya Magharibi yamefumbia macho na kutia pamba masikioni na kujifanya kutosikia vitendo hivyo vya kinyama vinavyofanywa na utawala wa Aal Saud.
Vyombo vya habari pia ambavyo vina mfungamano na madola ya Magharibi ambavyo hushupalia kila tukio la haki za binadamu katika eneo la Asia Magharibi, kikawaida vinatosheka tu na kutangaza habari ya mauaji na hatua za kunyongwa wapinzani nchini Saudia na siyo zaidi ya hapo.
Ukweli wa mambo ni kuwa, madola ya Magharibi yanayopigia debe suala la haki za binadamuu na kujifanya kuwa vinara na washika bendera wa kadhia hiyo, yamekuwa na undumakuwili na yanalitumia suala la haki za binadamu kama wenzo na fimbo ya kuzichapia zile nchi zinazoyapinga na zisizokubali kuburuzwa na madola hayo. Na ndio maana tunashuhudia yakinyamazia kimya na kutochukua hatua zozote za maana kuhusiana na ukiukaji wa haki za binadamu mkubwa unaofanyika katika baadhi ya mataifa ikiwemo Saudi Arabia.