Saudia na Kuwait kuwarejesha mabalozi wao Lebanon
Saudi Arabia na Kuwait zimeamua kuhuisha uhusiano wao wa kidiplomasia na Beirut, ambao uliingia doa mwaka jana kufuatia matamshi ya ukosoaji aliyotoa aliyekuwa waziri wa habari wa Lebanon kuhusiana na uchokozi na uvamizi wa kijeshi wa muungano wa kivita wa unaoongozwa na Saudia dhidi ya Yemen.
Gazeti la al-Liwaa linalochapishwa kila siku kwa lugha ya Kiarabu nchini Lebanon limeripoti kuwa, Waleed Bukhari, Balozi wa Saudia nchini Lebanon anatazamiwa kurejea Beirut ndani ya siku chache zijazo.
Gazeti hilo limeongeza kuwa, Kuwait pia inajiandaa kumrejesha balozi wake nchini Lebanon katika kipindi cha wiki chache zijazo; ikiwa ni katika jitihada za kufufua uhusiano wa Beirut na nchi wanachama wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi.
Oktoba mwaka jana, serikali ya Saudia ilimwita nyumbani balozi wake wa mjini Beirut na kumpa balozi wa Lebanon mjini Riyadh muda wa masaa 48 aondoke katika ardhi ya nchi hiyo, mbali na kusimamisha uingizaji nchini humo bidhaa zote zitokazo Lebanon.
Mivutano na mikwaruzano katika uhusiano wa Saudia na Lebanon ilishadidi Oktoba mwaka jana, kufuatia matamshi aliyotoa aliyekuwa waziri wa habari wa Lebanon, George Kordahi ya kulaani uchokozi na uvamizi wa muungano wa Saudia dhidi ya Yemen.
Kordahi alisema, uvamizi huo "hauna tija yoyote" na akasisitizia udharura wa kukomeshwa hujuma na mashambulio yanayofanywa na muungano wa kijeshi wa Saudia dhidi ya Yemen.
Msimamo huo wa Kordahi uliikasirisha sana Saudi Arabia na waitifaki wake katika Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi, na baadhi ya nchi hizo zikafuata kibubusa mkumbo huo wa Riyadh na kukata uhusiano na Lebanon.