Televisheni ya Saudia yarusha kipindi cha kumdhihaki Biden
Televisheni moja inayofadhiliwa na dola la Saudi Arabia imerusha kipindi cha kuchekesha, kilichoonekana kumdhihaki na kumdhalilisha Rais wa Marekani Joe Biden, huku uhusiano wa Washington na Riyadh ukiendelea kuporomoka.
Kwenye kipindi hicho cha "Studio 22" kilichorushwa hewani Jumatatu ya juzi na kanali ya televisheni ya MBC ya Saudi Arabia, muigizaji alimsawiri Biden kama mzee mkongwe, mwenye kusinzia ovyo na mwenye hulka ya kusahau.
Muigizaji huyo ambaye alikuwa anamuigiza Biden kana kwamba anahutubia vyombo vya habari katika Ikulu ya White House, alionekana akihangaika huku na kule jukwani, kiasi cha kurejeshwa kwa nguvu kwenye kipaza sauti na muigizaji mwingine mwanamke aliyekuwa akimuigiza makamu wake Kamala Harris.
Katika sehemu moja ya kipindi hicho cha kuchekesha, "Biden" alionekana kukanganyikiwa na kushindwa kutofautisha baina ya bara Afrika na nchi ya Uhispania, huku akilisahau jina la Rais wa Russia, Vladimir Putin na badala yake akamuita Harris.
Hii ni katika hali ambayo, uhusiano wa Saudi Arabia na Marekani unaendelea kudorora na kuporomoka vibaya. Mwezi uliopita wa Machi, gazeti la Wall Street Journal (WSJ) liliwanukuu maafisa wa Marekani na nchi za Asia Magharibi wakisema kuwa, Mrithi wa Ufalme wa Saudia, Mohammad bin Salman na Mrithi wa Ufalme wa Abu Dhabi katika Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) Sheikh Mohammed bin Zayed Al Nahyan wamekataa kupokea simu za Biden katika wiki za hivi karibuni.
Biden alitaka kuzishawishi Saudia na Imarati kuongeza kiwango cha uzalishaji wa mafuta ghafi ya petroli ili kupunguza bei ya bidhaa hiyo, iliyopanda kutokana na vikwazo vya Wamagharibi wakiongozwa na Marekani, dhidi ya mafuta ya petroli ya Russia.