Balozi wa Palestina London aitaka Magharibi kukomesha unafiki
-
Husam Zomlot
Mwakilishi wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina nchini Uingereza ameashiria kimya cha nchi za Magharibi mbele ya vitendo vya kikatili vinavyofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel katika Msikiti wa Al-Aqsa na kueleza kuwa, Palestina itakombolewa kutokana na uungaji mkono mkubwa wa watu huru duniani.
Katika wiki za hivi karibuni, askari wa utawala ghasibu wa Israel na walowezi wa Kizayuni walifanya mashambulizi dhidi ya Msikiti wa Al-Aqsa na waumini wa Kipalestina waliokuwa wakitekeleza ibada ya Swala na kujeruhi na kuua makumi miongoni mwao.
Hadi sasa Uingereza bado haijatoa tamko rasmi kuhusu hujuma na mashambulizi hayo. Wiki mbili zilizopita, msemaji wa Waziri Mkuu wa Uingereza, alijitoa kimasomaso na kutosheka kwa kueleza wasiwasi wake kuhusu yanayojiri huko Quds Tukufu.
Mwakilishi wa Palestina nchini Uingereza, Husam Zomlot aliyekuwa akizungumza katika maandamano yaliyokuwa yakipiga nara za "mauti kwa Israel" mbele ya ubalozi wa Israel mjini London, amesema: "Wakati Waisraeli wanapojeruhiwa, maafisa wa Uingereza na nchi za Magharibi kwa ujumla hukimbilia kupinga na kulaani tukio hilo; kwa nini wananyamaza kimya wakati mamia ya wanajeshi wa Israel wanaposhambulia Msikiti wa Al-Aqsa, ambao ni msikiti wa tatu kwa utakatifu katika Uislamu tena wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhani? Zomlot amehoji kwamba, Wamagharibi wanakuwa wapi wakati walowezi wa Kizayuni wanapowashambulia raia wa Palestina?
Mwakilishi wa Palestina nchini Uingereza amesema, wananchi wa Palestina hawana matumaini ya kuungwa mkono na nchi za Magharibi, lakini mamilioni ya walimwengu wanaunga mkono kadhia ya Palestina na wataendelea kupigania uhuru na haki za Wapalestina."
Mamia ya watu wa matabaka mbalimbali walikusanyika mbele ya ubalozi wa Israel mjini London kupinga ukatili na jinai zinazoendelea kufanywa na utawala wa Kizayuni katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina.

Waandamanaji katika maandamano hayo yaliyoitishwa na makundi yanayoiunga mkono Palestina ikiwemo Jumuiya ya Waislamu wa Uingereza na Kampeni ya Mshikamano na Palestina, wametoa wito wa kuzidishwa mashinikizo ya serikali ya Uingereza ili kuzuie uhalifu wa utawala wa Kizayuni.