Hamas yatuma salamu za hongera kwa kuachiwa huru mwanamapambano wa Kijapani
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i84158-hamas_yatuma_salamu_za_hongera_kwa_kuachiwa_huru_mwanamapambano_wa_kijapani
Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS na Harakati ya Wananchi kwa ajili ya Ukombozi wa Palestina zimetuma salamu za hongera kwa kuachiwa huru Fusako Shigenobu, mwanamama mtetezi na muungaji mkono wa Palestina ambaye alitumikia kifungo cha miaka 20 katika jela za Japan.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 29, 2022 07:46 UTC
  • Hamas yatuma salamu za hongera kwa kuachiwa huru mwanamapambano wa Kijapani

Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS na Harakati ya Wananchi kwa ajili ya Ukombozi wa Palestina zimetuma salamu za hongera kwa kuachiwa huru Fusako Shigenobu, mwanamama mtetezi na muungaji mkono wa Palestina ambaye alitumikia kifungo cha miaka 20 katika jela za Japan.

Fusako, mwenye lakabu ya "Maryam", ambaye ni mtetezi na muungaji mkono wa Palestina na mmoja wa waasisi wa Jeshi Jekundu la Japan, aliachiwa huru jana Jumamosi baada ya kutumikia kifungo cha miaka 20 jela na kulakiwa na familia yake pamoja na baadhi ya waandishi wa habari na wafuasi wake katika mji mkuu wa nchi hiyo Tokyo.

Kwa mujibu wa televisheni ya Al Mayadeen, msemaji wa Hamas Jihad Taha, amesema, kuachiwa huru Fusako Shigenobu, mpigania huru wa Kijapani, ambaye alikuwa akitumikia kifungo kwenye jela za Japan kwa sababu ya kuwatetea na kuwaunga mkono Wapalestina katika mapamabno dhidi ya Israel, kunachukuliwa kuwa ni ushindi kwa yeye mwenyewe na malengo matukufu ya Palestina.

Fusako Shigenobu, kabla na sasa

Harakati ya Wananchi kwa ajili ya Ukombozi wa Palestina imetoa taarifa ambayo sambamba na kutuma salamu za hongera na pongezi kwa kuachiwa huru mwanamapambano huyo wa kimapinduzi wa Japan na kutangaza kuwa watu wa Palestina hawatayasahau yaliyofanywa na mpambanaji huyo na wenzake katika Jeshi Jekundu la Japan kwa ajili ya Palestina.

Harakati ya Wananchi kwa ajili ya Ukombozi wa Palestina imewatolea mwito watetezi wa uhuru duniani kufuata mfano wa mwanamama huyo mwanamapinduzi wa Japan.../