Wiki ya kimataifa ya kuondoa mzingiro wa Ukanda wa Gaza
Wakati maadhimisho ya kimataifa ya kuondoa mzingiro uliowekewa Ukanda wa Gaza yakiwa yanakaribia, A'laa al-Batt'ah, mratibu wa harakati za kitaifa za kuondoa mzingiro wa Gaza ametoa wito kwa Wapalestina na watetezi wa uhuru duniani kote kushiriki katika shughuli na harakati za wiki ya kimataifa ya kuondolewa mzingiro wa Gaza ambayo inatazamiwa kuanza katika wiki ya mwisho ya mwezi huu wa Juni.
Kampeni ya kimataifa ya kuondoa mzingiro wa Gaza itafanyika sambamba na maadhimisho ya kumbukumbu ya siku askari wa utawala wa Kizayuni wa Israel walipowaua abiria waliokuwemo ndani ya meli ya MV Marmara ya Uturuki. Kampeni hiyo itakayojumuisha shughuli na harakati mbalimbali itafanyika kwa kaumlimbiu ya "Wiki ya Kimataifa ya Kuondoa Mzingiro wa Gaza".
Tangu mwaka 2007, Ukanda wa Gaza wa Palestina inayokaliwa kwa mabavu umewekewa mzingiro na jeshi la utawala haramu wa Israel; na vivuko vyote vya kuingilia na kutokea katika eneo hilo vimefungwa. Rafah, Karam Abu Salim na Beit Hanun, ndivyo vivuko vikuu na muhimu zaidi vya Ukanda wa Gaza, ambavyo kufungwa kwake kumekatisha mawasiliano baina ya wakaazi wa Gaza na ulimwengu wa nje na kuwafanya washindwe kufikishiwa bidhaa muhimu za mahitaji yao ya msingi ya kila siku. Kati ya vivuko vyote vya Ukanda wa Gaza, kufungwa kivuko cha Rafah, ambayo ndiyo njia kuu ya mawasiliano ya Gaza na ulimwengu wa nje kumesababisha hali mbaya sana ya kibinadamu na kiuchumi kwa eneo hilo la Palestina inayokaliwa kwa mabavu.
Katika miaka ya karibuni, Jumuiya na asasi zisizo za kiserikali zimeandaa misafara ya ardhini na baharini kwa madhumuni ya kufikisha misaada ya chakula, dawa, fueli na vifaa vya ujenzi huko Gaza, lakini katika matukio kadhaa, utawala wa Kizayuni wa Israel umewashambulia kwa risasi wanaharakati wa haki za binadamu au hata kuwaponda kwa vifaru na mabuldoza wafikishaji misaada ya kibinadamu ili kuufanya ulimwengu ughairi na kubadili uamuzi wa kuwapelekea misaada Wapalestina wa Gaza.
Itakumbukwa kuwa Rachel Corrie, kijana wa Kimarekani mwenye umri wa miaka 23, mwanachama wa Harakati ya Kimataifa ya Mshikamano (ISM) ya kuunga mkono Wapalestina aliuliwa kwa kupondwa na buldoza la jeshi la utawala wa Kizayuni alipojaribu kulizuia buldoza hilo lisibomoe nyumba za Wapalestina katika eneo la Rafah kusini mwa Ukanda wa Gaza.
Eneo la Ukanda wa Gaza lenye ukubwa wa kilomitamraba 365 wanaishi ndani yake watu wanaokaribia milioni mbili. Milioni moja kati ya Wapalestina hao ni wakimbizi ambao baada ya kupita miaka 50 wangali wanaishi kwenye kambi za wakimbizi za Ukanda wa Gaza. Tangu ulipoanza kuiwekea mzingiro Gaza, utawala haramu wa Kizayuni ulikuwa na lengo la kuuvunja na kuusambaratisha muqawama wa Kiislamu wa Wapalestina wa Gaza.
Baada ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina (HAMAS) kushinda uchaguzi wa bunge la Palestina uliofanyika mwaka 2006 utawala ghasibu wa Israel ulianza kuliandama eneo la Ukanda wa Gaza kwa mashambulio makali vikiwemo vita vitatu angamizi kwa lengo la kuupigisha magoti muqawama katika eneo hilo. Hata hivyo licha ya mashinikizo, mbinyo na vita hivyo vya Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza, eneo hilo dogo la ardhi ya Palestina limegeuka kuwa nembo ya muqawama na kusimama imara. Katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, eneo la Gaza limegeuzwa kuwa gereza lisilo na dari kwa Wapalestina ili kuwahilikisha na kuwaua ndani ya ardhi walikozaliwa. Hata hivyo hatua ya ulimwengu kuanzisha kampeni ya wiki ya kimataifa ya kuondoa mzingiro wa Gaza inathibitisha kuwa yangali hai matumaini ya watu wanaoendelea kusubiri siku ya kuhitimishwa uvamizi na kukaliwa kwa mabavu ardhi yao.../