Mvua na mafuriko yaua watu zaidi ya 300 nchini Pakistan
Watu wasiopungua 310 wamefariki dunia nchini Pakistan kutokana na mafuriko na matukio yanayohusiana na mvua kali zinazoendelea kunyesha nchini humo.
Mamlaka Taifa ya Kusimamia Majanga (NDMA) imetangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, wanawake na watoto wadogo 175 ni miongoni mwa wahanga wa majanga hayo ya kimaumbile, yaliyopelekea pia watu 300 kujeruhiwa.
Taarifa ya NDMA imeeleza kuwa, watu 64 wameaga dunia mashariki mwa mkoa wa Punjab, 62 kaskazini magharibi mwa mkoa wa Khyber Pakhtunkhwa, huku watu zaidi ya 70 wakipoteza maisha kusini mwa mkoa wa Sindh.
Mamlaka hiyo imeongeza kuwa, nyumba 8,979 na madaraja karibu 50 yameharibiwa au kusombwa na maji ya mafuruko hayo katika kona mbalimbali za nchi hiyo.

Habari zaidi zinasema kuwa, Jeshi la wanamaji la Pakistan linaendelea na operesheni za utoaji misaada kwa waathirika wa mafuriko sambamba na kuwahamisha watu wanaoishi kwenye maeneo hatarishi zaidi.
Mwaka uliopita pia, mamia ya watu walifariki dunia na kujeruhiwa na nyumba nyingi zilibomoka kutokana na mafuriko na maporomoko ya udongo yaliyosababishwa na mvua kali za msimu zilizonyesha katika maeneo mbalimbali ya Pakistan.
Mamlaka ya hali ya hewa ya Pakistan imetabiri kuwa, mvua kali zilizoanza kunyesha Juni 14 katika maeneo mbalimbali ya nchi zitaendelea kwa muda wa siku kadhaa zijazo.