Palestina: Ni kinaya kuteuliwa Israel kuongoza kamati ya UN
Afisa wa ngazi za juu wa Palestina ameitaja kama kichekesho na kinaya, hatua ya kuteuliwa utawala wa Kizayuni wa Israel kuwa mwenyekiti wa kamati ya Umoja wa Mataifa.
Hanan Ashrawi, ofisa mwandamizi wa Chama cha Ukombozi wa Palestina cha PLO amekosoa vikali kuteuliwa utawala haramu wa Israel kuongoza Kamati ya 6 ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, inayoshughulikia maswala ya kisheria ya baraza hilo.
Amesema ni kinaya kuteuliwa Israel kuongoza kamati hiyo ya sheria, katika hali ambayo ni utawala huohuo haramu ndio hauheshimu sheria za kimataifa. Hanan Ashrawi amesema haingii akilini kuteuliwa Israel kuongoza kamati ya sheria inayofaa kuhakikisha kuwa sheria za kimataifa zinatekelezwa ilhali utawala huo wenyewe unakiuka wazi wazi haki za msingi za binadamu. Ofisa huyo wa Palestina amefananisha kitendo hicho cha kuteuliwa Israel kuongoza kamati ya sheria ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kama dhihaka kwa mfumo wa sheria za kimataifa.
Utawala wa kizayuni wa Israel umeteuliwa kuongoza kamati hiyo katika hali ambayo, Jumapili iliyopita, shirika la kimataifa la Haki za Binadamu la Human Rights Watch liliitaka Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC ianze kuwafuatilia kisheria viongozi wa utawala huo haramu wanaofanya jinai za kivita. Taarifa hiyo ya Human Rights Watch iligusia pia jinai za kidhalimu zinazofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina hasa wanaotekwa nyara na utawala huo na kuitaka ICC iwapandishe kizimbani viongozi wa Israel wanaofanya jinai hizo.