HAMAS: Wapalestina wataendeleza mapambano ya ukombozi
(last modified Thu, 03 Nov 2022 11:40:12 GMT )
Nov 03, 2022 11:40 UTC
  • HAMAS: Wapalestina wataendeleza mapambano ya ukombozi

Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina (HAMAS) imesema wananchi wa Palestina wataendeleza kwa nguvu zote jitihada na mapambano ya kulikomboa kikamilifu taifa lao kutoka kwenye makucha ya utawala wa Kizayuni wa Israel.

HAMAS imesema hayo katika taarifa iliyoitoa kwa mnasaba wa kutimia miaka 105 tangu kutolewa Azimio la Balfour lililoandaa uwanja wa kuasisiwa utawala haramu wa Israel huko katika ardhi za Palestina zilizokuwa chini ya wakoloni wa Uingereza.

Taarifa ya HAMAS imeeleza kuwa: Azimio hilo la Uingereza, dhambi zao za kisiasa na mauaji ya halaiki ya watu wetu (Wapalestina), na kukanyagwa haki zetu ikiwemo haki ya kumiliki ardhi yetu, na uungaji mkono wenye upendeleo wa Marekani kwa utawala ghasibu, ni jitihada zilizogonga mwamba za kujaribu kufanikisha mradi wa Israel katika ardhi za Palestina.

HAMAS imeutaja mji mtukufu wa Quds na Msikiti Mtakatifu wa al-Aqsa kama kitovu cha mgogoro wa Wapalestina na utawala wa Tel Aviv unaofanya jitihada za kuyayauhudisha maeneo hayo matukufu ya Waislamu.

Wanamapambano wa HAMAS

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imeashiria jinai za kutisha zilizofanywa na Wazayuni dhidi ya Wapalestina tangu kutolewa Tangazo la Balfour na kueleza kuwa, kurejea wakimbizi wa Kipalestina katika ardhi za mababu zao ni haki yao ya msingi na halali, na isiyoweza kufanyiwa mjadala.

HAMAS yenye makao yake mjini Gaza imebainisha kuwa, maadhimisho ya mwaka huu ya kutimia miaka 105 tangu kutolewa Azimio la Balfour inajiri katika hali ambayo, wakazi wa Quds na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan wanaendeleza operesheni kabambe za kusimama kidete na kupambana dhidi ya Wazayuni maghasibu ili kuikomboa Palestina.

Tags