Hamas: Utawala wa Kizayuni hauwezi kubadili utambulisho wa Quds
Msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) amesema: Utawala wa Kizayuni wa Israel hauwezi kubadili utambulisho wa kihistoria wa Quds tukufu.
Msikiti wa al Aqsa ambao ni nembo kuu na ya asili ya utambulisho wa Kiislamu na Palestina katika mji wa Baitul Muqaddas siku zote unalengwa na hujuma na hatua za uharibifu za utawala haramu wa Israel unaoikalia Quds kwa mabavu.
Muhammad Hamadeh, Msemaji wa Hamas huko Quds inayokaliwa kwa mabavu amesema kuwa utawala wa Kizayuni katu hauwezi kubadili uhakika wa kihistoria na utambulisho wa mji wa Quds kwa kujenga makaburi ya uwongo katika eneo hilo linalokaliwa kwa mabavu.

Hamadeh amesisitiza kuwa jitihada kubwa zinazofanywa na utawala ghasibu wa Israel ili kubadili athari na alama za kihistoria za Quds inayokaliwa kwa mabavu kupitia kupora ardhi za mji huo, kuanzisha mabustani ya Torati na kujenga makaburi ya uwongo ni jinai mpya za Wazayuni na ni ukikaji wa wazi wa sheria na maazimio yote ya Umoja wa Mataifa. Amesema, utawala wa Kizayuni unafanya hivyo kutokana na kufeli na kukata kwake tamaa.
Msemaji wa Hamas kwa mara nyingine tena amesisitiza kuwa harakati hiyo inapinga mipango hiyo na miradi ya kuiyahudisha Quds na kwamba wananchi wa Palestina wanashikamana na ardhi yao na wataendelea kutetea matukufu yao kwa kutumia njia na nyenzo zote hadi pake ardhi hizo zitakapokombolewa kikamilifu na kuangamizwa maghasibu wa Kizayuni.