Dec 10, 2022 03:13 UTC
  • OIC yalaani jinai za utawala wa Kizayuni huko Jenin

Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) imelaani hujuma ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya mji na kambi ya wakimbizi ya Jenin, mauaji ya Wapalestina wanne na pia hujuma dhidi ya Msikiti wa Ibrahim na shule za Palestina.

Ni baada ya Wapalestina wanne kuuliawa shahidi kwa kupigwa risasi katika shambulio la wanajeshi wa utawala haramu wa Israel kwenye mji na kambi ya wakimbizi ya Jenin, kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu imetoa taarifa ikisema, jinai hizo pamoja na hujuma za hapo awali ambazo zimekuwa zikifanyika mara kwa mara, zinapaswa kuchunguzwa na kufuatiliwa kisheria.

Taarifa hiyo imesema, kwa mara nyingine tena OIC inasisitiza "mshikamano na uungaji mkono wake kwa mapambano ya wafungwa wa Kipalestina na inatoa wito kwa mashirika ya kutetea haki za binadamu na taasisi za kimataifa kuchukua hatua za haraka za kuachiliwa huru Nasser Abu Hamid, mfungwa wa Kipalestina ambaye hali yake ya kiafya ni mbaya."

Askari wa Israel wakimnyanyasa Mpalestina

Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu imesema, utawala ghasibu wa Israel unawajibika kwa matokeo ya hujuma na jinai zinazoendelea kufanywa dhidi ya wananchi wa Palestina.

OIC pia imeitaka jamii ya kimataifa hususan Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutekeleza majukumu yake ya kukomesha uchokozi wa utawala wa Kizayuni na kuwaunga mkono watu wa Palestina.

Wapalestina wasiopungua 216 wameuawa shahidi kwa kuupigwa risasi na wanajeshi wa utawala ghasibu wa Israel tangu mwanzoni mwa mwaka huu wa 2022; 164 kati yao wameuawa Ukingo wa Magharibi na 52 katika Ukanda wa Gaza. 

Tags