UNRWA: Israel inakiuka sheria za kimataifa kwa kuzuia misaada kwa Gaza
-
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA)
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) limekosoa kuendelea kuwekewa vikwazo vya misaada katika Ukanda wa Gaza na kueleza kuwa, utawala ghasibu wa Israel kama utawala unaoukalia kwa mabavu hautekelezi wajibu wake kwa mujibu wa sheria za kimataifa za kibinadamu.
Kwa mujibu wa UNRWA, kwa kuendelea kuzuia uingiaji wa misaada katika Ukanda wa Gaza, utawala wa Israel unakiuka sheria za kimataifa za kibinadamu; utawala wa Israel unakataa kutekeleza majukumu yake ya kisheria kama mamlaka inayoikalia kwa mabavu.
Hapo awali UNRWA ilionya kwamba mvua kubwa na ukosefu wa makazi vimesababisha hali ya kibinadamu kwa wakaazi wa Gaza kuwa mbaya sana, na kuzilazimisha familia kutafuta hifadhi katika maeneo ya muda.