Unicef: Ugonjwa wa surua wauwa watoto 15 Yemen
Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (Unicef) limetangaza kuwa katika kipindi cha miezi saba iliyopita watoto 15 wa kiyemen wameaga dunia kwa surua(Measles).
Shirika la Unicef limesema katika taarifa yake kwamba: watoto wasiopungua 1,400 katika mikoa saba ya Yemen ikiwemo mkoa wa Aden kusini mwa nchi hiyo walishukiwa kupatwa na ugonjwa wa surua kati ya mwezi Januari na Julai mwaka huu.
Taarifa ya unicef imeendelea kubainisha kuwa, shirika hilo na washirika wake imezisaidia mamlaka husika za Yemen kutoa chanjo za polio kwa watoto wenye umri sifuri hadi miaka 10; na kutoa chanjo za surua kwa wale wenye umri kuanzia miezi 6 hadi miaka 10.
Surua ni ugonjwa wa virusi unaoambukiza sana unaoenea kwa watoto. Ugonjwa huo husababisha vipele vinavyoambata na maumivu ngozini, maumivu ya macho, homa, misuli kukakamaa, na kukohoa sana kwa karibu kila mtu anayeambukizwa na virusi.
Yemen iliathiriwa na hali ya mchafukoge na vita tangu Septemba mwaka 2014 wakati wapiganaji wa Kiouthi walipodhibiti sehemu kubwa ya nchi hiyo ikiwemo mji mkuu Sana'a. Aidha Muungano vamizi huko Yemen chini ya uongozi wa Saudi Arabia ulianzisha uvamizi nchini humo mwezi Machi 2015 kwa lengo la kuirejesha madarakani serikali kibaraka ya Abd- Rabb Mansour Hadi.
Vita hivyo vilivyotimiza miaka nane sasa vimesababisha janga kubwa zaidi la kibinadamu kuwahi kushuhudiwa duniani huku mamilioni ya wananchi wa Yemen wakiathiriwa na njaa.