Hamas: Wapalestina hawataiacha Israel itekeleze njama zake
(last modified Tue, 13 Dec 2022 02:54:28 GMT )
Dec 13, 2022 02:54 UTC
  • Hamas: Wapalestina hawataiacha Israel itekeleze njama zake

Mkuu wa ofisi ya kisiasa ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema Wapalestina katu hawatouruhusu utawala haramu wa Israel utekeleza njama na mipango yake michafu dhidi ya mji mtakatifu wa Quds na Masjidul Aqsa.

Ismail Haniya amesema hayo katika hotuba aliyoitoa jana Jumatatu kwa mnasaba wa kuadhimisha miaka 35 tangu ilipoasisiwa harakati hiyo ya mapambano ya Kiislamu huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni.

Amesisitiza kuwa, wananchi wa Palestina wataendelea kusimama kidete dhidi ya njama za Wazayuni na kusisitiza kuwa, Quds itasalia kuwa kipaumbele cha kwanza kwa Hamas na taifa zima la Palestina katika zama na pahala popote.

Haniya amebainisha kuwa, kutumia muqawama na mapambano kwa ajili ya kukabiliana na uvamizi na ukaliaji wa mabavu wa ardhi zao unaofanywa na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel ndiyo njia pekee ya kukabiliana na mipango ghalati ya Wazayuni.

Kiongozi huyo wa Hamas ameeleza bayana kuwa, utawala haramu wa Kizayuni wa Israel umo katika hali ya kudhoofika sana na katu hauwezi kuwa na ushawishi tena katika eneo la Asia Magharibi.

Uungaji mkono wa Palestina katika Kombe la Dunia Qatar

Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina amesema bayana kwamba, njama za utawala vamizi wa Israel za kujipenyeneza katika eneo la Asia Magharibi hakuwezi kubadilisha udiriki na mwamko wa mataifa ya eneo hili.

Kadhalika Haniya amewapongeza wananchi wa nchi za Kiarabu kwa kuonyesha wazi wazi uungaji mkono wao kwa taifa la Palestina katika mashindano ya kandanda ya Kombe la Dunia ya FIFA yanayofanyika nchini Qatar.

Aidha amekosoa vikali hatua ya baadhi ya mataifa ya Kiarabu ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala ghasibu wa Israel na kubainisha kwamba, hatua hiyo katu siyo kwa maslahi ya Palestina na Quds.

Tags