Jamii ya kimataifa yaikosoa Bahrain kupiga marufuku al-Wefaq
Mashirika ya kutetea haki za binadamu yamelaani hatua ya utawala wa Bahrain ya kukipiga marufuku chama kikuu cha upinzani nchini humo cha al-Wefaq.
Shirika la Human Rights First lenye makao makuu yake nchini Marekani limesema kupigwa marufuku chama hicho kwa muda usiojulikana ni mwendelezo wa wimbi jipya la utawala wa Manama wa kutaka kuvifunga mdomo vyama vya upinzani nchini. Brian Dooley, ofisa wa shirika hilo amesema kuwa, kusimamishwa shughuli za chama kikuu cha upinzani nchini humo kunadhihirisha namna serikali ya Bahrain inavyokusudia kufunga majukwaa na njia zote za wananchi kujieleza na kutoa lalama zao. Taarifa ya Human Rights First imeongeza kuwa, mkondo huo wa serikali ya Manama kuvinyamazisha vyama vya siasa ni hatari na unaweza kuchochea zaidi mgogoro wa kisiasa katika nchi hiyo ndogo ya Ghuba ya Uajemi. Jana Jumanne, Wizara ya Sheria ya utawala wa Aal-Khalifa ilitangaza kusimamisha shughuli zote za chama cha al-Wefaq, siku moja baada ya kumkamata Nabeel Rajab, mkuu wa kituo cha haki za binadamu nchini humo.
Siku chache zilizopita, Mfalme Hamad bin Issa Aal Khalifa alitoa dikrii ya kubadilishwa baadhi ya vipengee vya kisheria kuhusu vyama vya kisiasa na kupiga marufuku shughuli za siasa zinazoendeshwa na vituo vya kidini na wanazuoni nchini humo.