Mufti Mkuu wa Oman aunga mkono kususiwa utawala haramu wa Israel
Mufti Mkuu wa Oman ameunga mkono mpango wa Bunge la nchi hiyo wa kususiwa utawala haramu wa Israel unaotenda jinai kila uchao huko Palestina.
Sheikh Ahmed bin Hamad Al Khalili amesisitiza kuwa: Tunaunga mkono muswada wa marekebisho ya kifungu cha 10 cha sheria ya kuharamisha na kupiga marufuku kushirikiana na utawala wa Kizayuni wa Israel ili upasishwe rasmi.
Mufti wa Oman ameongeza kuwa: Tunaunga mkono mpango huo kutokana na kuendelea hujuma, na uvamizi wa utawala ghasibu wa Israel na kukanyagwa haki za wananchi madhulumu wa Palestina.
Majuzi Baraza la Ushauri la Oman liliikabidhi Kamati wa Kutunga Sheria na Kulinda Haki ya nchi hiyo, muswada wa marekebisho ya kifungu cha 10 cha sheria ya kuharamisha na kupiga marufuku kushirikiana na utawala wa Kizayuni wa Israel ili upasishwe rasmi. Hatua hiyo ya Bunge la Oman, ni katika kukamilisha Dikrii ya Kifalme nambari 9/72 ya Oman kuhusu kuususia utawala wa Kizayuni na ambayo ilitolewa na Sultan Qaboos.
Dikrii hiyo ya Kifalme inatilia mkazo marufuku ya kuweka mikataba ya aina yoyote ile ya moja kwa moja na isiyo ya moja kwa moja baina ya taasisi na watu wa Oman na utawala wa Kizayuni wa Israel. Dikrii hiyo imepiga marufuku pia miamala na ushirikiano na mashirika yote ambayo yana manufaa au matawi yao katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni ambazo zimepachikwa jina bandia la Israel.