Mwanazuoni wa Bahrain: Ni haramu kuwauzia ardhi Mayahudi
(last modified Sat, 07 Jan 2023 07:10:50 GMT )
Jan 07, 2023 07:10 UTC
  • Mwanazuoni wa Bahrain: Ni haramu kuwauzia ardhi Mayahudi

Imamu Sala ya Ijumaa katika mji wa Al-Diraz nchini Bahrain, amesema kuwauzia ardhi Wayahudi ni sawa na kuiuza nchi na ni haramu.

Septemba 2020, viongozi wa Bahrain na wa utawala haramu wa Kizayuni  wa Israel walisaini makubaliano ya kuanzisha uhusiano wa kawaida katika hafla iliyofanyika Ikulu ya White House mbele ya rais wa zamani wa Marekani Donald Trump.
Kufuatia kusainiwa makubaliano hayo ya kuanzishwa uhusiano wa kawaida kati ya Bahrain na utawala haramu wa Israel, duru za habari ziliripoti mpango wa kutengwa eneo maalumu la Mayahudi katika mji mkuu wa nchi hiyo Manama.
Kwa mujibu wa tovuti ya habari ya Al-Ahad, Sheikh Muhammad Sanqur, Imamu wa Sala ya Ijumaa katika mji wa Al-Diraz, Bahrain, amezungumzia katika khutba zake za Sala ya Ijumaa ya jana, habari zilizotangazwa kuhusu uuzaji ardhi na majengo kwa Wayahudi huko Bahrain na kubainisha kwamba kuwauzia ardhi maghasibu na wanyang'anyi wa ardhi ya Wapalestina ni sawa na kuiuza nchi.

Imamu wa Sala ya Ijumaa katika mji wa Al-Diraz amesema, kuwauzia ardhi na majengo Wayahudi ni haramu na akasisitizia haja ya kukabiliana na njama chafu zinazofanywa kwa ajili ya kufanikisha mpango huo.

Wachambuzi wa masuala ya Bahrain wanaashiria hatua zinazochukuliwa na utawala wa Al Khalifa za kuimarisha uhusiano na utawala ghasibu wa Kizayuni na kulifanya kuwa suala kawaida kuwepo kwa wazayuni hao katika nchi za Kiarabu zinazopakana na Ghuba ya Uajemi na kutoa indhari kwamba, suala hilo linaonekana kuwa ni pana zaidi ya uhusiano wa kawaida tu baina ya pande mbili.../