HAMAS: Jinai za kila uchao za Israel hazitapita hivi hivi
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) sambamba na kusema kuwa imesikitishwa na kitendo cha kuuawa shahidi vijana wawili wa Kipalestina na utawala haramu wa Israel, imeonya kuwa, jinai za kila uchao za utawala huo wa Kizayuni hazitapita hivi hivi.
Taarifa iliyotolewa jana Ijumaa na HAMAS imesema kuwa, utawala ghasibu wa Israel unabeba dhima ya hujuma na uvamizi wake wa kila leo dhidi ya Wapalestina, na kwamba jinai hizo hazitapita bila kugunduliwa.
HAMAS imesema imesikitishwa na hatua ya jeshi katili la Israel ya kuwaua shahidi vijana wawili wa Kipalestina huko katika mji wa Jenin huko Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na kaskazini mwa mji wa Quds.
Wazayuni siku ya Alkhamisi waliwaua shahidi Wapalestina wawili, Habib Mohammad Ikmail huko Qabatiya umbali wa kilomita sita kusini mwa mji wa Jenin; na Samir Ouni Harbi Aslan huko Qalandiya kaskazini mwa mji wa Quds.
Kila uchao wanajeshi wa utawala wa Kizayuni kwa visingizio mbalimbali huwashambulia wananchi madhulumu wa Palestina kwa kuwaua, kuwajeruhi au kuwatia nguvuni.
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) imesisitiza katika taarifa hiyo kuwa, Wapalestina wana haki ya msingi ya kupambana na uvamizi wa utawala ghasibu wa Israel na kupigania uhuru, ukombozi na mamlaka yao ya kujitawala, kama linavyoashiria Azimio Nambari 37/43, la Disemba 3, 1982.