Wanaharakati watoa mwito wa kuachiliwa huru wafungwa wa kisiasa Bahrain
Wanaharakati wengi na watumiaji wa mitandao ya kijamii nchini Bahrain wametoa mwito wa kuachiliwa huru wafungwa wa kisiasa wa nchi hiyo.
Wanaharakati hao wamesisitiza kuwa, wafungwa wa kisiasa nchini Bahrain wanakabiliwa na mazingira mabaya katika magereza ya nchi hiyo.
Makundi na asasi za kutetea haki za binadamu nchini Bahrain zimesisitiza kuwa, kuna haja kwa jamii ya kimataifa kuingilia kati na kuhitimisha madhila na mateso yanayowakabili wafungwa wa kisiasa nchini humo.
Mwito huo unatolewa katika hali ambayo, asasi za kutetea haki za binadamu zimekuwa zikitahadharisha mara kwa mara kuhusiana na ukandamizaji mkubwa unaofanywa nchini Bahrain na vyombo vya usalama dhidi ya raia na kutaka kukomesha vitendo hivyo.
Utawala wa kiimla nchini Bahrain umekuwa ukikandamiza wapinzani tangu ulipotumia mkono wa chuma mwaka 2011 kwa msaada wa utawala wa Saudi Arabia kupambana na maandamano na vuguvugu la umma la kupigania mageuzi ya kidemokrasia.
Tangu wakati huo Bahrain imekumbwa na vuguvugu la harakati za mapinduzi ya wananchi dhidi ya utawala wa ukoo wa Aal Khalifa. Wananchi wa Bahrain wanataka kuwa huru, kutekelezwa uadilifu, kukomeshwa ubaguzi na kuingia madarakani serikali itakayochaguliwa kwa njia ya kidemokrasia.
Mbali na adhabu za vifungo, utawala wa Aal Khalifa umewafutia uraia pia mamia ya Wabahrain katika kesi bandia zilizoendeshwa kwa umati na mahakama za utawala huo wa kifalme.