Mzingiro wa Saudia unahatarisha maisha ya watoto 3,000 Yemen
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i93726-mzingiro_wa_saudia_unahatarisha_maisha_ya_watoto_3_000_yemen
Vita vya Saudia dhidi ya Yemen na mzingiro mkali dhid ya nchi hiyo masikini ya Kiarabu vinaweza kusababisha vifo vya maelfu ya watoto wanaougua saratani, shirika la kutetea haki za binadamu la Yemen limeonya.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 06, 2023 04:29 UTC
  • Mzingiro wa Saudia unahatarisha maisha ya watoto 3,000 Yemen

Vita vya Saudia dhidi ya Yemen na mzingiro mkali dhid ya nchi hiyo masikini ya Kiarabu vinaweza kusababisha vifo vya maelfu ya watoto wanaougua saratani, shirika la kutetea haki za binadamu la Yemen limeonya.

Shirika la Haki za Wanawake na Watoto la Entisaf limesema katika taarifa yake kwa mnasaba wa Siku ya Saratani Duniani kwamba zaidi ya watoto 3,000 wa Yemen ambao wamepata saratani kutokana na uvamizi wa Saudia na kuzingirwa kwa bahari, nchi kavu na angani nchini humo sasa wako katika hatari kubwa ya kifo.

Kundi hilo la kutetea haki za binadamu limekosoa mashirika ya kimataifa na vyombo vingine vinavyohusika kwa kutowajali wagonjwa wa saratani wa Yemeni katika miaka iliyopita.

Enfisaf ameongeza kuwa visa vya saratani ya damu vinaongezeka miongoni mwa watoto wa Yemen, akisema visa vya watoto wanaougua saratani ya damu vimeongezeka kutoka 300 hadi 700 katika mji mkuu Sana'a kutokana na matumizi ya silaha zilizopigwa marufuku kimataifa zinazotolewa na Marekani  na Uingereza na kutumiwa vitani na muungano unaoongozwa na Saudia dhidi ya Yemen.

Shirika hilo limeongeza kuwa, takriban watoto 1,000 pia wanaaminika kuwa na saratani ya damu katika maeneo mengine ya Yemeni kutokana na sababu hizo hizo.

Watoto, wahanga wakuu wa vita vya Yemen

Entisaf imeashiria uhaba mkubwa wa dawa zinazohitajika kwa ajili ya matibabu ya wagonjwa waliogundulika kuwa na saratani kwa sababu ya mashambulizi na mzingiro wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia, ikieleza kuwa watoto wengi hupoteza maisha kutokana na hali hiyo.

Shirika hilo la kutetea haki za binadamu limebainisha kuwa matatizo ya kiuchumi yanayosababishwa na uvamizi na vizuizi vya kijeshi vinavyoendelea vimewazuia wagonjwa wadogo wa saratani kwenda kutafuta matibabu nje ya nchi, likitoa wito wa kufunguliwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Sana'a kwa madhumuni ya kibinadamu.

Hatimaye imesema Saudi Arabia na waitifaki wake wanawahibika kikamilifu kwa jinai na ukiukaji wote unaofanywa dhidi ya taifa la Yemen hususan watoto na kuitaka jumuiya ya kimataifa kubeba dhima ya kisheria na kibinadamu kwa ukiukaji huo dhidi ya raia.

Saudi Arabia, kwa ushirikiano na washirika wake wa Kiarabu na msaada wa silaha na vifaa kutoka Marekani na mataifa mengine ya Magharibi, ilianzisha vita vya kinyama dhidi ya Yemen mwezi Machi 2015.

Lengo lilikuwa ni kuangamiza vuguvugu la muqawama la Ansarullah, ambalo limekuwa likiendesha masuala ya serikali bila ya kuwepo serikali inayofanya kazi nchini Yemen na kusimamisha tena utawala wa kirafiki wa Riyadh wa Abd Rabbuh Mansour Hadi.

Muungano unaoongozwa na Saudi Arabia umeshindwa kufikia malengo yake yoyote, na kuwaacha mamia ya maelfu ya Wayemen wakiuawa na kusababisha mzozo mbaya zaidi wa kibinadamu duniani.