Wapalestina 42 wameuawa shahidi tangu kuanza mwaka huu wa 2023
Kwa akali Wapalestina 42 wameuawa shahidi na jeshi la utawala haramu wa Israel tangu kuanza mwaka huu wa 2023.
Hiyo ni baada ya vijana 6 wa Kipalestina kuuawa shahidi katiika kipindi cha masaa 48 yaliyopita huko Jericho na Nablos.
Wizara ya Afya ya Palestina imetangaza kuwa, hadi kufikia sasa na tangu kuanza mwaka huu jumla ya Wapalestina 42 wameuawa shahidi kwa kupigwa riisasi na wanajeshi wa Israel katika maeneo mbalimbali ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, miongoni mwa waliouawa shahidi yupo mwanamke na mtoto mmoja huku makumi ya wengine wakijeruhiwa katika matukio mbalimbali ya hujuma na mashambulio ya wanajeshi wa utawala ghasibu wa Israel.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, Umoja wa Mataifa umetangaza katika ripoti yake kwamba mwaka uliopita wa 2022 ulikuwa mwaka wa umwagaji damu zaidi katika ardhi za Palestina katika kipindi cha miaka 16 iliyopita.
Tangu mwaka 2008 utawala wa Israel umeanzisha vita vinne katika ardhi ya Palestina na kuua karibu watu 4,000 ambao robo yao ni watoto wadogo.
Mapigano yanayotokea baina ya Wapalestina na utawala wa Kizayuni husababisha vifo vya watu wengi wasio na hatia hasa wanawake na watoto wadogo. Watoto wa Kipalestina wanauliwa shahidi hata kama hawashiriki kivyovyote vile katika mapigano hayo.