Ahmed Aboul Gheit: Quds inakabiliwa na hatari ya kubadilishwa utambulisho
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu ametahadharisha kuwa, mji wa Quds si tu kwamba, umekaliwa kwa mabavu na Wazayuni maghasibu bali eneo hilo takatifu linakabiliwa na hatari ya kubadilishwa utambulisho wa kihistoria, Kiislamu na Kikristo.
Ahmed Aboul Gheit amesema hayo katika mkutano wa "Quds-Uthabiti na Ustawi" na kuonya kwamba, licha ya kuwa Quds iko katika dhamira za Waarabu lakini hii leo eneo hilo mbali na kukaliwa kwa mabavu linakabiliwa na hatari ya kubadilishwa utambulisho wake wa kihistoria.
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League) ameongeza kuwa, utawala haramu wa Israel unafanya njama za kuliyahudisha eneo hilo kupitia ukandamizaji na kubomoa nyumba za Wapalestina.
Kadhalika kiongozi huyo wa ngazi za juu wa Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League) amebainisha kuwa, Quds inakaliwa kwa mabavu lakini hakuna mtu anayeweza kubadilisha ukweli na uhakika wa historia na njama zote zinazofanyika kwa ajili ya kuuyahudisha mji huo mtakatifu hazina natija ghairi ya kuzidi vitendo vya utumiaji mabavu.
Vitendo vya kuyavunjia heshima matukufu ya Kiislamu huko Palestina vinafanyika katika hali ambayo, viongozi wa nchi za Kiarabu na jamii ya kimataifa wameendelea kunyamaza kimya na kutochukua hatua zozote za maana za kukabiliana na vitendo hivyo vinavyokinzana na utu na ubinadamu.
Utawala wa Kizayuni ambao unaungwa mkono kikamilifu na Marekani katika hatua zake hizo haramu umedhamiria kubadilisha muundo wa kijiografia na kidemografia wa maeneo ya Palestina; ili kuyazayunisha maeneo hayo na kuhakikisha unazihodhi na kuzidhibiti kikamilifu ardhi za Wapalestina.