Damascus: Kusimamisha kwa muda vikwazo vya Marekani dhidi ya Syria hakutoshi
-
Bassam al Sabagh
Mwakilishi wa Kudumu wa Syria katika Umoja wa Mataifa amesema kuwa kusimamishwa kwa upande mmoja na kwa muda baadhi ya vikwazo vya serikali ya Marekani dhdi ya Damascus hakutasadia kutondoa taathira hasi za muda mrefu za vikwazo hivyo.
Wizara ya Fedha ya Marekani awali ilitangaza kuwa, inasimamisha kwa miezi kadhaa vikwazo dhidi ya Syria ili kuandaa mazingira ya kutolewa baadhi ya huduma na hatua za kibinadamu baada ya tetemeko kubwa la ardhi kuyaathiri maeneo ya Syria na Uturuki.
Marekani imesimamisha baadhi ya vikwazo dhidi ya Syria baada ya viongozi wa Umoja wa Mataifa na mashirika ya misaada ya kimataifa kutahadharisha kuwa vikwazo vya Marekani vinakwamisha juhudi za kutolewa misaada kwa waathiriwa wa zilzala huko Syria.
Shirika la habari la IRNA limeripoti kuwa, Bassam al Sabagh amesema katika kikao maalumu cha Umoja wa Mataifa kuhusu misaada ya kibinadamu kwa waathiriwa wa tetemeko la ardhi huko Syria kwamba raia zaidi ya 250,000 wa Syria wamepoteza makazi yao kufuatia zilzala hiyo.
Sabagh ameongeza kuwa, Syria inaunga mkono suala la kupelekwa nchini humo misaada ya kibinadamu kutokea upande wa kaskazini-magharibi mwa nchi na kupitia vivuko vyote vya mpakakani na ndani ya nchi kwa muda wa miezi mitatu.
Mwakilishi wa Syria katika Umoja wa Mataifa amesema kuwa, mwendo wa kinyonga wa utumaji misaada ya kibinadamu kwa nchi yake ni matokeo ya vikwazo na hatua za upande mmoja dhidi ya Damascus. Ameongeza kuwa, haipasi kuwaacha manusura wa tetemeko hilo la ardhi waage dunia kwa kupigwa na baridi kali, njaa, ukosefu wa dawa na makazi salama.