Changamoto za mazingira zimeathiri eneo zima la Asia Magharibi
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, taathira na changamoto za kimazingira katika eneo hazijaathiri nchi chache pekee, bali zimeathiri eneo zima la Asia Magharibi na kuongeza kuwa uamuzi wa nchi yoyote wa kutoshirikiana na nchi nyingine katika uwanja huo hautaisadia lolote.
Hossein Amirabdollahian, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, katika ujumbe wake kwa mkutano wa kwanza wa kitaifa wa masuala ya diplomasia na changamoto za mazingira zinazovuka mipaka ya mataifa, uliofanyika mjini Tehran Jumapili, amesema kwamba uwezo wa mazingira kujijenga upya baada ya kuharibiwa na kiwango cha uharibifu unaofanywa na mwanadamu kwenye mazingira hayo haviendani kwa kasi sawa.
Amir Abdollahian amesema uharibifu huo mkubwa wa mwanadamu katika mazingira umeibua changamoto nyingi kwa jamii ya mwanadamu katika ngazi za kitaifa, kieneo na kimataifa.
Mkuu huyo wa siasa za kigeni za Iran amesema uingiliaji wa binadamu katika mzunguko wa asili wa mazingira na uharibifu wake mkubwa ukiwemo usimamizi usiofaa wa rasilimali za maji, nishati na uharibifu wa ardhi umezua wasiwasi mkubwa kuhusu mafanikio na maendeleo pamoja na usalama wa jamii ya mwanadamu duniani. Kwa upande mwingine, uingiliaji wa kijeshi, vita na ugaidi umebuni pembetatu ya kutisha, ambayo, pamoja na athari zake zote hasi, imesababisha uharibifu mkubwa wa mazingira na miundombinu katika mataifa tofauti.
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amesema kuwa katika eneo la Asia Magharibi, vita na migogoro ya miongo michache iliyopita imedhoofisha au kuharibu kabisa mifumo na miundombinu ya kikanda ya ushirikiano katika nyanja mbalimbali, ikiwa ni pamoja na mazingira.