Jihadul-Islami ya Palestina: Kila risasi inayowalenga wanamapambano inawaongezea nguvu
Feb 28, 2023 22:51 UTC
Mjumbe wa ofisi ya kisiasa ya harakati ya Jihadul-Islami ya Palestina amesema, kila risasi inayofyatuliwa kuwalenga wanamapambano wa Palestina inawaongezea nguvu zaidi wanamapambano hao.
Makumi ya walowezi wa Kizayuni katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan Jumapili usiku walishambulia kitongoji cha Wapalestina cha Hawara kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na vijiji vya kandokando yake na kuchoma moto mali na magari ya Wapalestina.
Khalid al-Batash amesisitiza katika mahojiano na kituo cha habari cha Saut al-Quds kwamba tangu utawala haramu wa Kizayuni wa Israel ulipounda baraza lake la mawaziri la wanasiasa wenye misimamo ya kufurutu ada umekuwa ukijiwa na njozi za kudhani kwamba kwa kushadidisha jinai zake utaweza kuvunja irada ya muqawama na kuwatia hofu wanamapambano wa Palestina.
Al-Batash amesema jibu la Wapalestina kwa uchokozi wa utawala huo ghasibu linatolewa kwa uwazi kabisa na akaongeza kwamba, operesheni za kishujaa za wanamapambano wa Kipalestina na uanzishaji wa brigedi za muqawama katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan zinaendelea kuongezeka.
Mjumbe huyo mwandamizi wa ofisi ya kisiasa ya Jihadul-Islami amesema, "kila risasi inayofyatuliwa na adui kuwalenga wananchi wa Palestina inaongeza nguvu na azma yetu ya kuendeleza muqawama na ukombozi wa Palestina".
Al-Batash amebainisha kuwa, jinai ya utawala haramu wa Kizayuni ya kuchoma moto nyumba ni jinai kwa maana yake halisi; ni jinai inayofanywa kwa uungaji mkono wa jeshi la Kizayuni ikiandamana na kimya cha jamii ya kimataifa.
Mjumbe huyo wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Jihadul-Islami ya Palestina ameongeza kuwa, licha ya juhudi za kimataifa za kubadilisha ukweli wa mambo, suala la Palestina litaendelea milele kubaki kuwa suala la kimsingi la Umma (wa Kiislamu).../