Katibu Mkuu wa UN atembelea Iraq
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i94624-katibu_mkuu_wa_un_atembelea_iraq
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres Jumatano ameanza ziara nchini Iraq lengo likiwa ni kusisitiza mshikamano na kuunga mkono juhudu za nchi za kuleta amani, haki za binadamu na maendeleo endelevu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 02, 2023 01:10 UTC
  • Katibu Mkuu wa UN atembelea Iraq

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres Jumatano ameanza ziara nchini Iraq lengo likiwa ni kusisitiza mshikamano na kuunga mkono juhudu za nchi za kuleta amani, haki za binadamu na maendeleo endelevu.

Ziara ya mwisho ya Katibu Mkuu Guterres nchini Iraq ilikuwa miaka sita iliyopita, na alipofika Baghdad alipokelewa na Naibu Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya nje Fued Hussein ambapo walifanya mkutano wa pamoja na waandishi wa habari.

Katika hotuba yake Katibu Mkuu Guterres aliipongeza serikali ya Iraq kwa kuwaruhusu wananchi wa Iraq walio nje ya ncho hiyo kurejea na kusema Umoja wa Mataifa unaunga mkono kikamilifu juhudi zote za kuhakikisha nchi hiyo inakuwa na mustakabali wa amani na ustawi na taasisi zake zinaunganishwa na demokrasia.

Pia amezungumzumzia changamoto zinazowakabili wananchi wa nchi hiyo ikiwemo uhaba wa maji na athari za mabadiliko ya tabianchi na kusema “Moyo wangu unavunjika nikiona wakulima wanaacha ardhi zao na mazao ambayo wamekuwa wakilima kwa miaka. Uhaba wa maji nchini Iraq umechangiwa na kupungua kwa uingiaji kutoka nje, usimamizi usio endelevu wa maji, na sasa athari za mabadiliko ya tabianchi. Ni tishio linalohitaji umakini wa kimataifa.”

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akiwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq Fuad Hussein punde baada ya kuwasili Baghdad

Katika kupata suluhu ya changamoto hiyo amesema mkutano Umoja wa Mataifa wa Maji utakaofanyika baadaye mwezi huu mjini New York utajadili mengi kuhusu changamoto ya maji huku akidhibitisha kuelewa ni kwa namna gani suala la uhakika wa maji ni muhimu kwa nchi hiyo.

Katika ziara yake hiyo, mbali na mkutano wake na Waziri Mkuu Mohammed Shia’, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa pia atakutana na viongozi mbalimbali wa serikali.

Leo Alhamisi Katibu Mkuu Guterres atatembelea kambi ya Wakimbizi wa Ndani kaskazini mwa nchi hiyo na kufanya mazungumzo na wakazi wa kituoni hapo.