Kuibuka mifarakano miongoni mwa wanajeshi wa Kizayuni
Kikosi kamili cha makomando watajika wa jeshi la Anga la Israel kwa jina la " Sheldag" kimetangaza kuwa hakipo tayari kutekeleza majukumu yake ya kijeshi.
Muungano tawala wa mrengo wa kulia wenye misimamo ya kuchupa mipaka unaoongozwa na Benjamin Netanyahu tangu uingie madarakani hadi sasa umechukua maamuzi na kutekeleza hatua mbalimbali; ambazo kwa mtazamo wa wapinzani na rais wa utawala wa Kizayuni zitapelekea utawala huo kukabiliwa na mgogoro mkubwa wa ndani na hata kukaribia vita vya ndani.
Shirika la habari la Palestina la SAMA limeripoti kuwa, katika kuendelea malalamiko na upinzani kwa mpango wa Waziri Mkuu wa Israel "Benjamin Netanyahu" kwa jina la mpango wa marekebisho ya sheria za mahakama mashuhuri katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu kama mpango wa mapinduzi wa "Bibi" umepelekea kundi la makomando wa utawala wa Tel Aviv kutangaza kujitoa katika serikali hiyo yenye misimamo mikali ya utawala wa Kizayuni.
Wiki iliyopita, askari na maafisa wa jeshi wa ngazi ya juu wa vikosi vya akiba ndani ya jeshi na askari jeshi wa anga walikosoa hatua zinazotekelezwa na serikali ya Netanyahu; ambapo wamesema kuwa watakaidi kulitumikia jeshi iwapo hatua hizo zitaendelea.
Wanajeshi hao ambao ni pamoja na marubani na askari jeshi maafisa wa ngazi ya juu huku wakihudumu katika kitengo cha intelijinsia ya jeshi na ulinzi wa anga wamesaini barua na kusisitiza kuwa uhudumu wao jeshini ni lazima uzingatie sheria za utawala wa Kizayuni na kile kinachojulikana kama "uhuru wa mawazo" pasina woga wowote na kwamba masuala yote hayo yatatoweka kama utawala wao utakuwa wa kidikteta. Uamuzi wa serikali ya Netanyahu wa kubadili muundo wa sheria za mahakama za utawala huo umeibua mivutano ya kisiasa na hitilafu za kimitazamo kati ya muungano tawala na mrengo wa upinzani.