Mash'al: Kuanzisha uhusiano na Israel umeisababishia Palestina dhiki
(last modified Sun, 05 Mar 2023 10:58:57 GMT )
Mar 05, 2023 10:58 UTC
  • Mash'al: Kuanzisha uhusiano na Israel umeisababishia Palestina dhiki

Kiongozi wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina (HAMAS) nje ya nchi ameyakosoa baadhi ya madola ya Kiarabu kwa kuanzisha uhusiano wa kawaida na Israel na kusisitiza kuwa, ushirikiano na utawala huo wa Kizayuni haujakuwa na matokeo mengine ghairi ya kuwasababishia Wapalestina dhiki na matatizo.

Khalid Mash'al alisema hayo jana usiku na kuongeza kuwa, kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na utawala huo haramu kumeusababishia majanga na balaa chungu nzima ulimwengu wa Kiarabu. Amesema taharuki na mivutano baina ya Palestina na Israel huenda ikishtadi katika mwezi mtukufu wa Ramadhani unaoanza baada ya chini ya wiki tatu.

Ameeleza bayana kuwa, mikataba ya mapatano iliyosainiwa na nchi za Kiarabu kwa ajili ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na Israel haijawa na tija wala faida yoyote kwa Waarabu na umma wa Kiislamu.

Mash'al amesema, "Lengo kuu la kuanzisha uhusiano na Israel ni kuyasambaratisha mataifa ya Kiarabu. Kufanya wa kawaida uhusiano na Israel ni sawa na kulipiga jambi kwa nyuma taifa la Palestina."

Kiongozi huyo wa Harakati ya HAMAS nje ya nchi amesisitiza kuwa, taifa la Palestina litaendeleza muqawama na mapambano yake dhidi ya Israel ili kuhakikisha linapata haki zake na linakomesha kukaliwa kwa mabavu ardhi yake na mwishowe litapata ushindi.

Maandamano ya kupinga uhusiano na Israel

Mwaka 2020, nchi za Kiarabu za Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Bahrain, Morocco na Sudan chini ya mashinikizo ya Marekani zilichukua hatua ya kupatana na Israel ili kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala huo haramu wa Kizayuni unaokikalia kwa mabavu kibla cha kwanza cha Waislamu.

Kiongozi wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS nje ya nchi ameongeza kuwa, madola hayo ya Kiarabu yamejikurubisha kwa Israel licha ya pingamizi kutoka kwa wananchi, wanaharakati na makundi ya muqawama ya nchi hizo.

 

 

Tags