Ansarullah yalaani kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu
Harakati ya Ansarullah ya Yemen imelaani vitendo vya kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu nchini Denmark na katika nchi nyingine za Ulaya.
Katika ujumbe wa Twitter jana Alkhamisi, Mohammad Abdul Salam, Msemaji wa Ansarullah amekosoa vikali wimbi hilo la kuvunjiwa heshima Kitabu Kitukufu cha Waislamu katika nchi za Denmark na Sweden.
Ametoa mwito kwa mataifa ya Kiislamu kusimama kidete dhidi ya wafuasi wa makundi yenye misimamo mikali ya mrengo wa kulia katika nchi hizo za Ulaya kwa kuyavunjia heshima Matukufu ya Kiislamu.
Abdu Salam amesema inasikitisha kuona nchi hizo zinazojidai kuwa vinara na watetezi wa haki za binadamu, zinafanya uchokozi huo wa kuumiza kwa makusudi hisia za Waislamu duniani, kwa kisingizio cha uhuru wa kujieleza.
Siku chache zilizopita, kundi lenye chuki dhidi ya Uislamu la Patrioterne Gar Live, lilichoma moto nakala ya Qur'ani Tukufu huko Copenhagen, mji mkuu wa Denmark.
Aidha mapema mwaka huu, Rasmus Paludan, mwanasiasa mwenye misimamo mikali wa Denmark alichoma moto nakala ya Qur'ani Tukufu karibu na Ubalozi wa Uturuki mjini Stockholm huku akiwa analindwa na polisi ya Sweden.
Kadhalika Edwin Wagensveld, mwanasiasa mwingine wa siasa kali za mrengo wa kulia wa Uholanzi, na kiongozi wa kundi la chuki dhidi ya Uislamu la Pegida, alirarua kurasa za Qur’ani Tukufu huko The Hague, mji mkuu wa Uholanzi. Video ya Wagensveld kwenye Twitter ilionyesha kuwa alichoma kurasa zilizochanwa za Qur’ani Tukufu.
Vitendo hivi vimelaaniwa vikali na Waislamu pamoja na nchi za Kiislamu duniani ambapo serikali za Sweden na Uholanzi zimekosolewa kwa kuunga mkono vitendo hivyo viovu.