Qatar: Kuwaunga mkono Wapalestina ni kipaumbele katika sera zetu za nje
(last modified Fri, 14 Apr 2023 06:59:27 GMT )
Apr 14, 2023 06:59 UTC
  • Qatar: Kuwaunga mkono Wapalestina ni kipaumbele katika sera zetu za nje

Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar amesema, kuwaunga mkono wananchi wa Palestina ni kipaumbele cha kwanza cha sera za nje za nchi hiyo.

Kwa mujibu wa chaneli ya habari ya Al Jazeera, Muhammad bin Abdulrahman Al Thani, Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar ametangaza kuwa, kuwaunga mkono Wapalestina na kuunga mkono kusimama kwao imara kukabiliana na uchokozi wa utawala ghasibu wa Kizayuni ni kipaumbele kikuu katika sera za nje za nchi hiyo.
 
Muhammad bin Abdurrahman Al Thani ameongeza kuwa matukio ya hivi karibuni ya Baitul Muqaddas yanatoa indhari kubwa; na Qatar inaunga mkono muqawama wa Wapalestina.
 
Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar amebainisha kuwa ulimwengu utachukua misimamo ya kiundumakuwili kuhusiana na matukio ya Msikiti uliobarikiwa wa Al-Aqsa.

Afisa huyo wa Qatar amesisitiza kuwa, hujuma za mtawalia zinazoendelea kufanywa na utawala wa Kizayuni na hatua za kujaribu kubadilisha hadhi ya kihistoria na kisheria ya Msikiti wa Al-Aqsa kwa kuzuia kufanywa itikafu, kuwashambulia waumini wanaokwenda kusali na kuyafanya mashambulizi dhidi yao kama kitu cha kawaida kwa lengo la kugawanya matumizi ya msikiti huo kwa sehemu na wakati hakukubaliki.

 
Msikiti wa Al-Aqsa takriban kila siku unashuhudia hujuma na uvamizi mkubwa unaofanywa na walowezi wa Kizayuni wanaoingia kwa halaiki msikitini humo kwa ulinzi na uungaji mkono wa wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel.
 
Mji wa Quds, ambao ndani yake kipo kibla cha kwanza cha Waislamu cha Msikiti wa Al-Aqsa, ni sehemu isiyotenganika na Palestina na ni moja ya maeneo matatu muhimu zaidi kwa utakatifu katika Uislamu.../