Nakba ya Palestina iliyogeuzwa kuwa Nakba ya Israel!
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i97462-nakba_ya_palestina_iliyogeuzwa_kuwa_nakba_ya_israel!
Licha ya mashinikizo na kampeni kubwa iliyofanywa na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel na Marekani ya kuzishawishi nchi mbalimbali, wanachama wa Umoja wa Mataifa siku ya Jumatatu waliadhimisha kwa mara ya kwanza kumbukumbu ya mwaka wa 75 wa maangamizi ya kizazi cha wananchi madhulumu wa Palestina katika tukio la Siku ya Nakba.
(last modified 2026-05-13T14:18:38+00:00 )
May 17, 2023 04:30 UTC
  • Nakba ya Palestina iliyogeuzwa kuwa Nakba ya Israel!

Licha ya mashinikizo na kampeni kubwa iliyofanywa na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel na Marekani ya kuzishawishi nchi mbalimbali, wanachama wa Umoja wa Mataifa siku ya Jumatatu waliadhimisha kwa mara ya kwanza kumbukumbu ya mwaka wa 75 wa maangamizi ya kizazi cha wananchi madhulumu wa Palestina katika tukio la Siku ya Nakba.

Siku chache kabla ya maadhimisho hayo, Marekani na utawala wa Kizayuni zilifanya kampeni ya kuzishawishi nchi mbalimbali duniani zisishiriki katika hafla ya kumbukumbu ya Siku ya Nakba; na hata zikajaribu kuzishinikiza nchi hizo na kudai kwamba kufanyika kwa hafla hiyo kutakwamisha juhudi za kutafuta suluhu ya kisiasa ya kadhia ya Palestina.
 
Hafla ya kumbukumbu ya Siku ya Nakba iliandaliwa na Ofisi ya Palestina ya Utazamaji wa Kudumu katika Umoja wa Mataifa ikishirikiana na Kamati ya Kutetea Haki Zisizoweza Kupokwa za Watu wa Palestina katika Umoja wa Mataifa, kwa msaada wa Tawi la Haki za Wapalestina katika idara ya masuala ya kisiasa na uletaji amani.
Maadhimisho ya Siku ya Nakba UN

Katika hafla hiyo, wawakilishi wa Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika, Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi, Kundi la 77, Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, Vuguvugu la Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote na Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu kila mmoja alitoa ujumbe na salamu za kuwaunga mkono watu wanaodhulumiwa wa Palestina kutokana na jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel.

 
Rosemary DiCarlo, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia masuala ya kisiasa, alitangaza katika hafla hiyo: "kwa mujibu wa ripoti ya Ofisi ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu, tangu mwaka 2005 wakati ofisi hii ilipoanza kurekodi takwimu za wahanga wa Palestina, mnamo mwaka uliopita idadi kubwa zaidi ya Wapalestina waliouawa walikuwa wa Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu".
Mahmoud Abbas akihutubia UN maadhimisho ya Siku ya Nakba

Mahmoud Abbas, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina yeye katika hotuba yake aliyotoa kwenye hafla hiyo alisema, Uingereza na Marekani ndizo zinazobeba dhima ya moja kwa moja kisiasa na kimaadili kwa tukio la Nakba na akazihutubu nchi hizo kwa kuziambia: "Nyinyi mlipoamua kuweka utawala mwingine katika ardhi yetu ya kihistoria kwa ajili ya malengo yenu maalumu ya kikoloni, mlishiriki katika kulifanya mhanga taifa letu".

 
Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina alimalizia hotuba yake kwa kutaka uanachama wa Israel katika Umoja wa Mataifa usimamishwe au utawala huo haramu ulazimishwe kutekeleza maazimio na maamuzi yaliyopitishwa na taasisi hiyo ya kimataifa. 
 
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limeidhinisha azimio la kuunga mkono Palestina kuadhimisha kumbukumbu ya Nakba katika Umoja wa Mataifa kwa wingi wa kura 90 zilizounga mkono dhidi ya kura 30 zilizopinga na 47 za wanachama walioamua kutopiga kura.
Maafa ya Nakba

Mnamo Novemba 2022, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio la kuadhimisha kumbukumbu ya miaka 75 ya Siku ya Nakba.

 
Siku ya Nakba (Yaumun-Nakba) ni jina linalotumiwa na Wapalestina na wanaowaunga mkono kuashiria kumbukumbu ya kuhamishwa kwa nguvu mamia ya maelfu ya Wapalestina katika ardhi za Palestina na kuasisiwa utawala haramu na bandia wa Israel mnamo tarehe 14 Mei 1948, na huwa wanafanya maombolezo katika siku hiyo.
 
Katika usiku wa manane wa kuamkia tarehe 14 Mei, 1948, wanajeshi wa Uingereza, ambayo hadi wakati huo ilikuwa ikiikoloni Palestina, waliwapatia Wayahudi silaha na suhula zao zote na kuondoka katika ardhi ya nchi hiyo. Kutokana na hatua hiyo ya Uingereza, David Ben-Gurion, ambaye alikuwa mkuu wa Shirika la Mayahudi Ulimwenguni na Wakala wa Kiyahudi wakati huo, alitangaza mbele ya shakhsia 37 wa Kiyahudi kuasisiwa kwa utawala bandia wa Israel katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na akasema, "dola" la Israel linathibitisha rasmi kuwepo kwake kuanzia tarehe 15 Mei.
Kiongozi wa Wazayuni Ben Gurion

Kufuatia tangazo hilo, siku ya tarehe 15 Mei, 1948, magenge ya kigaidi ya Mayahudi, likiwemo la Hagana, Ashten, na Palmach, ambayo yalikuwa yakisimamiwa na kupewa mafunzo na Waingereza, yalianzisha mashambulizi ya kinyama dhidi ya miji na vijiji vya Palestina.

 
Wapalestina waliohamishwa kwa nguvu katika ardhi yao kwenye siku hiyo ya Nakba walikimbilia nchi jirani ikiwemo Jordan, Lebanon, Syria na pia Misri, na mpaka leo wanaishi katika kambi za wakimbizi wakisubiri siku ya kurudi makwao.
Wapalestina wakihama makazi yao ya asili bila hiari

Tarehe 15 Mei 1948 ni siku ya janga na maafa kwa watu wote wa Palestina ndani na nje ya ardhi hiyo; ni siku inayotambuliwa kwa jina la "Siku ya Nakba" ikiwa ndio mwanzo wa uvamizi na ukaliaji ardhi kwa mabavu uliofanywa na vuguvugu la Kizayuni na kubaki bila makazi Wapalestina baada ya kuhamishwa katika ardhi za mababa na mababu zao.

 
Katika siku zilizofuata baada ya Siku ya Nakba ya mwaka 1948, Wapalestina wasiopungua elfu 15 waliuawa shahidi na wengine laki saba na nusu walifukuzwa kwa kuhamishwa katika nchi yao. Idadi hiyo ilikuwa zaidi ya nusu ya watu wa Palestina wakati huo. Kwa jumla, asilimia 70 ya Wapalestina walifukuzwa au kulazimishwa kuondoka katika makazi yao ya asili.
 
Kuanzia mwaka 1948 hadi 1950 ilipovamiwa rasmi na kuanza kukaliwa kwa mabavu Palestina, zaidi ya miji na vijiji 530 vya Wapalestina vilibomolewa. Sehemu kubwa ya ubomoaji huo ililenga kuhakikisha kuwa Wapalestina waliohamishwa hawawezi kurudi tena kwenye makazi yao. Kwa muda wa miaka 75 sasa, zaidi ya Wapalestina 100,000 wameuawa shahidi kwa risasi za moja kwa moja walizofyatuliwa na Wazayuni na wengine milioni moja wamekamatwa.
 
Janga chungu na la kutisha ya Siku ya Nakba limesababisha mgogoro wa muda mrefu zaidi na wa kusikitisha zaidi wa kisiasa na wa hali mbaya ya kibinadamu kuwahi kushuhudiwa ulimwenguni katika kipindi cha miaka 100 sasa, kujitokeza mvurugiko mkubwa wa amani katika eneo, uvamizi na ukaliaji ardhi kwa mabavu ulioratibiwa, kuporwa kidhalimu ardhi ya Palestina, mauaji ya kimbari ya Wapalestina na kukiukwa haki za wazi kabisa za kiutu za wakazi wa asili wa ardhi hiyo tukufu kwa muda wa miaka 75 sasa.
 
Lakini licha ya Wapalestina wapatao milioni moja kuhamishwa katika makazi yao mwaka 1948 na wengine zaidi ya 200,000 baada ya vita vya Juni 1967, idadi ya Wapalestina hadi mwishoni mwa 2022 ilipindukia milioni 14 na laki tatu, hali inayoonyesha kuwa kutoka mwaka 1948 hadi leo, idadi ya Wapalestina imeongezeka mara 10; na hilo ni pigo na kushindwa kukubwa zaidi kwa utawala wa Kizayuni, kwa sababu ghaya na lengo kuu na la msingi la utawala huo kwa miongo kadhaa sasa, limekuwa ni kuufuta kikamilifu utambulisho wa Wapalestina.
Machungu ya Nakba wanayoendelea kuyahisi Wapalestina

Isitoshe, mlingano wa Muqawama umeufanya utawala wa Kizayuni ukiri kuwa baada ya vita vya mwaka 1967, Waisraeli hawajawahi kushinda vita vingine vyovyote vile. Hata katika vita vya siku 5 huko Gaza, baada ya kukiri Wazayuni kwamba hawana uwezo wa kukabiliana na makombora ya muqawama, waliamua kutafuta wapatanishi ikiwemo Misri kwa ajili ya kusimamisha mapigano.

 
Kila mwaka utawala wa Kizayuni ulikuwa ukiadhimisha siku ulipoivamia na kuanza kuikalia kwa mabavu Palestina kama siku ya kuasisiwa Israel, lakini mwaka huu, utawala huo umekumbana na vizuizi viwili katika ufanyaji wa sherehe hizo: Cha kwanza ni kwamba, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, kwa mara ya kwanza limeitambua siku hiyo kuwa siku ya Nakba kama walivyoomba Wapalestina; na cha pili ni kuwa, kuvurumishwa karibu makombora 1,500 kutoka Gaza kuelekea Palestina inayokaliwa kwa mabavu wakati wa vita vya siku 5 kupitia operesheni iliyoongozwa na kamandi ya pamoja ya makundi ya muqawama ya kulipiza kisasi cha mauaji ya wanachama wa harakati ya Jihadul-Islami ya Palestina, kuliukosesha utawala wa Kizayuni fursa ya kufanya sherehe hizo. Lakini mbali na hayo, kuundwa baraza la mawaziri la wazayuni wenye misimamo mikali wakiongozwa na Netanyahu na vilevile kuchukua hatua nchi za Kiislamu na Kiarabu za eneo ya kufanya suluhu na mapatano kumeufanya utawala wa Kizayuni utengwe zaidi kikanda na kimataifa, mbali na kutelekezwa na hata waungaji mkono wake wa Magharibi.../