Arab League yatahadharisha:Jamii ya kimataifa imepuuza kadhia ya Palestina
(last modified Wed, 14 Jun 2023 07:44:55 GMT )
Jun 14, 2023 07:44 UTC
  • Arab League yatahadharisha:Jamii ya kimataifa imepuuza kadhia ya Palestina

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League) ametahadharisha kuhusu hatua ya jamii ya kimataifa ya kupuuza suala la Palestina chini ya kivuli cha utawala wa Kizayuni wenye misimamo mikali wa mrengo wa kulia.

Wanajeshi wa Israel wamezidisha mashambulizi dhidi ya Quds, Msikiti wa al Aqsa na katika maeneo mengine ya Palestina baada ya kuingia madarakani kwa mara nyingine tena Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel. 

Hujuma za Wazayuni dhidi ya msikiti wa al Aqsa 

Ahmad Aboul Gheit Katibu Mkuu wa Arab League aliyasema hayo jana katika mazungumzo yake na Tor Wennesland Mratibu Maalumu wa Umoja wa Mataifa katika mchakato wa amani wa Mashariki ya Kati katika makao makuu ya Jumuiya ya Nchi za Kiarabu huko Cairo Misri. Pande mbili zilibadilishana mawazo kuhusu matukio ya karibuni katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na juhudi za kurejesha amani. 

Aboul Gheit ametahadharisha kuhusu hatua ya jamii ya kimataifa ya kutozingatia suala la Palestina na pande mbili hizo pia zimetilia mkazo udharura wa kuupatia ufumbuzi mzozo baina ya Palestina na Israel. 

Taarifa ya Jumuiya ya Nchi za Kiarabu imeongeza kuwa mipango ya ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi katika ardhi ya Palestina inaweza kuvuruga juhudi za kuipatia ufumbuzi kadhia ya Palestina.  

Aboul Gheit aidha ametahadharisha kuhusu hali tete iliyopo katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu na kusisitiza kwamba kuna uwezekano wa kuzuka upya mvutano baina ya pande mbili.