Wazayuni waushambulia tena Msikiti wa al-Aqsa
Askari wa utawala haramu wa Israel na walowezi wa Kizayuni wameshambulia tena Msikiti Mtukufu wa al-Aqsa.
Msikiti wa al-Aqsa, ikiwa nembo kuu ya utambulisho wa Kiislamu na Palestina katika mji mtukufu wa Beitul Muqaddas, daima umekuwa ukilengwa na vitendo vya uharibifu vya utawala unaokalia kwa mabavu eneo hilo takatifu.
Kwa mujibu wa tovuti ya habari ya al-Ahad, leo Alkhamisi asubuhi idadi kubwa ya walowezi wa Kizayuni kwa mara nyingine tena wameushambulia Msikiti wa al-Aqsa katika hatua ya kichochezi na kichokozi huku wakiungwa mkono na vikosi vya usalama na jeshi la utawala huo ghasibu.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, walowezi wa Kizayuni walifanya desturi zao za kidini zinazojulikana kwa jina la "Talmudi" kwa ajili ya kuchokoza na kuwakera kwa makusudi wananchi Waislamu wa Palestina.
Mara kwa mara, walowezi wa Kizayuni huushambulia Msikiti wa al-Aqsa na kujaribu kubadilisha muundo wa kijamii na hadhi ya mahali hapo patakatifu.
Wavamizi wa Kizayuni wanataka kufikia lengo hilo ovu kwa kutumia kila mbinu wanayoweza.
Katika kukabiliana na mashambulizi na jinai za utawala wa Kizayuni katika Msikiti wa al-Aqsa, makundi ya mapambano ya Palestina yamekuwa yakilenga kwa makombora vitongoji vya walowezi wa Kizayuni karibu na mpaka wa Ukanda wa Ghaza na kaskazini mwa ardhi hizo zinazokaliwa kwa mabavu.
Makundi ya wapiganaji wa Kipalestina yanasisitiza kuwa Msikiti wa al-Aqsa ni mstari wao mwekundu na kwamba mashambulio yoyote ya maadui dhidi yake yatakabiliwa na jibu kali.